29 wakufa maji, 41 watoweka baada ya feri yao kuzama Indonesia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46554-29_wakufa_maji_41_watoweka_baada_ya_feri_yao_kuzama_indonesia
Kwa akali watu 29 wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya feri kuzama karibu na kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia, huku hatima ya makumi ya wengi ikisalia kitendawili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2018 03:00 UTC
  • 29 wakufa maji, 41 watoweka baada ya feri yao kuzama Indonesia

Kwa akali watu 29 wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya feri kuzama karibu na kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia, huku hatima ya makumi ya wengi ikisalia kitendawili.

Wizara ya Uchukuzi ya Indonesia imesema kuwa, watu 29 wamekufa maji katika ajali hiyo, huku wengine 41 wakitoweka. Taarifa ya wizara hiyo imesema watu 69 hata hivyo wameokolewa katika ajali hiyo, iliyotokea katika maji ya kisiwa cha Selayar, kusini mwa mkoa wa Sulawesi.

Ajali hiyo ya jana Jumanne imefanyika wiki chache baada ya feri nyingine iliyokuwa imebeba abiria kupita kiasi kuzama katika Ziwa Toba katika mkoa wa kaskazini mwa Indonesia wa Sumatra, ambapo watu wapatao 200 walipoteza maisha.

Boti yazama Indonesia

Ajali za namna hii zimekuwa zikitokea mara kwa mara nchini Indonesia na kusababisha maafa makubwa. Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwaka 2016, watu 54 walipoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama karibu na kisiwa cha Batam, nchini humo.

Ajali kubwa ya majini kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni nchini humo ni ile ya mwaka 2009, ambapo watu 330 walifariki dunia baada ya feri yao kuzama karibu na kisiwa cha Sulawesi.