Ufaransa yatwaa Kombe la Dunia 2018
Timu ya taifa ya soka ya Ufaransa imetwaa Kombe la Dunia la soka baada ya kuigaragaza Croatia mabao 4-2 katika mchezo wa fainali uliokuwa wa kusisimua.
Ufaransa iliyoingia mechi hiyo ikisaka ubingwa wa dunia kwa mara ya pili tangu 1998, ilitangulia kwenye mechi na goli la kwanza dakika ya 18 kufuatia mkwaju wa Antoine Griezmann ulioelekezwa wavuni na Mario Mandzukic aliyejifunga.
Mandzukic, shujaa dhidi ya Uingereza nusu fainali kwa kuipa goli la ushindi muda wa ziada, alimiminiwa lawama kwa kujifunga na kuwa mchezaji wa kwanza kupiga mpira hadi lango lake katika fainali ya Kombe la Dunia.
Uongozi wa Ufaransa ulidumu kwa dakika 10 pekee kwani winga matata wa Croatia anayeichezea Inter Milan Ivan Perisic, alifyatua kombora ndani ya sanduku na kukatiza sherehe za Ufaransa.
Pande zote zilionyesha dalili za kutofungana hadi dakika ya 37 pale Perisic alipounawa mpira wa kupinda wa Antoine Griezmann na kusababisha penalti.
Mfungaji Griezmann hakuchelea kuipa Ufaransa uongozi kwa kumduwaza kipa wa Croatia Subasic aliyeng'aa kwa kupangua matuta mechi za awali dhidi ya Denmark na Urusi.
Magoli ya Paul Pogba na Kylian Mbappe kipindi cha pili yaliikabidhi Ufaransa Kombe la Dunia mbele ya rais wake Emmanuel Macron na maelfu ya mshabiki ugani Luzhniki.
Baada ya kutolewa hatua ya makundi 2002, kufungwa na Italia 2006 kwenye fainali, kukumbwa na sakata kikosini 2010, na kutemwa na Ujerumani katika robo fainali 2014, hatimaye the Blues, chini ya Didier Deschamps wamefanikiwa jaribio lao Urusi 2018 kwa kuikung'uta Croatia 4-2 muda wa kawaida.
Licha ya kuwa katika timu iliyolazwa kwenye fainali, juhudi za nahodha wa timu hiyo Luka Modric hazikusahaulika kwani amekabidhiwa mpira wa dhahabu kwakuwa mchezaji bora wa Kombe hili.
Mwingine aliyetunukiwa ni kipa wa Ubelgiji Thibaut Coutois aliyenyakua tuzo ya glovu za dhahabu kwa kuwa mdajaki bora Urusi.
Ingawa Uingereza ilimaliza nafasi ya nne, mfungaji wake Harry Kane alitia kapuni kiatu cha dhahabu kwani mabao ya Mbappe ya Griezmann hayakufikia sita aliyofunga Kombe hili.