EU yapinga mashinikizo ya Marekani kuitenga Iran
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya amesema EU haiwezi kuburuzwa na Marekani na kushinikizwa kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Federica Mogherini amesema umoja huo umekataa kuunga mkono mashinikizo yaliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, juu ya ya kuitenga Iran.
Amesema nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimeafikiana kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa zinaendelea kuwa na ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya amefafanua kuwa, "Tumejitolea kama EU kuendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya Iran. Tunaamini kwamba, kuendelea kulindwa na kutekelezwa mapatano hayo ya kimataifa ni kwa maslahi ya usalama wetu, wa kieneo na wa dunia kwa ujumla."
Baada ya Trump kuiondoa Marekani kwenye JCPOA mnamo Mei 8, kufuatia ombi la nchi za Ulaya la kutaka JCPOA ilindwe, Iran iliafiki kuzipa fursa mpya nchi zilizosalia katika makubaliano hayo, kwa sharti kwamba ziweze kudhamini maslahi ya Tehran kivitendo, wakati wa kurejea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kuanzia mwezi ujao wa Agosti.
Tayari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeishtaki Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ, kufuatia hatua hiyo ya Washington iliyo kinyume cha sheria ya kuiwekea tena Tehran vikwazo vya upande mmoja.