Sergey Lavrov: Marekani haitaki kutokomeza silaha zake za kemikali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47415-sergey_lavrov_marekani_haitaki_kutokomeza_silaha_zake_za_kemikali
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema kuwa Marekani inapinga kuangamiza silaha zake za kemikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 13, 2018 08:08 UTC
  • Sergey Lavrov: Marekani haitaki kutokomeza silaha zake za kemikali

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema kuwa Marekani inapinga kuangamiza silaha zake za kemikali.

Lavrov ameyasema hayo wakati akiashiria vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Russia na kuongeza kwamba, katika hali ambayo Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali OPCW limethibitisha kuwa maghala ya silaha za kemikali za Russia yametokomezwa, Washington bado haijakamilisha mchakato huo. Kadhalika Sergey Lavrov amebainisha kwamba, Russia ilitumia miaka mitatu kutokomeza maghala yake ya silaha hizo na suala hilo likathibitishwa na Shirika la OPCW, na akaongeza kwamba Marekani pia ilitakiwa kukamilisha zoezi hilo katika muda sawa na ule uliotumiwa na Russia lakini haikufanya hivyo. 

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amebainisha kwamba Marekani inakusudia kuchelewesha zoezi la kutokomeza silaha zake za kemikali hadi mwaka 2020 na kusisitiza kwamba Marekani inapinga kutokomezwa silaha za kemikali. Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kwamba, vikwazo vipya dhidi ya Russia kuhusiana na matumizi ya silaha za kemikali vitaanza kutekelezwa tarehe 22 ya mwezi huu. Inafaa kuashiria kuwa, Marekani imekuwa ikizilazimisha nchi nyingine duniani hususan zile zisizokubali siasa zake kutokomeza silaha za kemikali, katika hali ambayo yenyewe inamiliki maghala makubwa ya silaha hizo ndani na nje ya Marekani.