Mgogoro wa Marekani na Uturuki waendelea
Katika kuendelea mzozo kati ya Washington na Ankara, Rais Donald Trump wa Marekani amemtaja, Andrew Brunson, padri wa Kimarekani anayeshikiliwa nchini Uturuki kwa tuhuma za ujasusi, kuwa ni mateka.
Kwa mara nyingine Trump ameitishia Uturuki kutokana na hatua yake ya kuendelea kumshikilia padri huyo anayetuhumiwa kufanya ujasusi. Kupitia ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter rais huyo wa Marekani amesema kuwa Marekani haitolipa chochote kwa ajili ya kuachiliwa huru Brunson na badala yake itapunguza uhusiano wake na Uturuki. Alkhamisi iliyopita, Steven Mnuchin, Waziri wa Fedha wa Marekani alisisitiza kwamba, iwapo Andrew Brunson hatoachiliwa huru, basi Ankara itakabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi.
Brunson anayetuhumiwa kufanya ujasusi na kushiriki katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli ya tarehe 15 Julai 2016 nchini Uturuki, anaendelea kushikiliwa katika kifungo cha nyumbani nchini humo. Tarehe Mosi Agosti mwaka huu, serikali ya Marekani sambamba na kuzitaja tuhuma zinazomkabili padri huyo kuwa ni bandia na kufuatia kutoachiliwa kwake huru, iliwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Uturuki ambao ni Waziri wa Sheria na Mambo ya ndani wa nchi hiyo. Baada ya hatua hiyo Washington ilizipandishia ushuru bidhaa za chuma na aluminiam zinazozalishwa na Uturuki na hivyo ikawa imefungua vita vya kiuchumi dhidi ya Ankara.