Erdogan: Marekani imeanzisha jaribio la mapinduzi ya kiuchumi dhidi ya Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47539-erdogan_marekani_imeanzisha_jaribio_la_mapinduzi_ya_kiuchumi_dhidi_ya_uturuki
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema nchi yake haitasalimu amri mbele ya vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea nchi yake kutokana na kushikiliwa mhubiri Mkristo wa Kimarekani. Erdogan ameituhumu Marekani kuwa inatekeleza jaribio la mapinduzi ya kiuchumi dhidi ya nchi yake.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Aug 19, 2018 02:42 UTC
  • Erdogan: Marekani imeanzisha jaribio la mapinduzi ya kiuchumi dhidi ya Uturuki

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema nchi yake haitasalimu amri mbele ya vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea nchi yake kutokana na kushikiliwa mhubiri Mkristo wa Kimarekani. Erdogan ameituhumu Marekani kuwa inatekeleza jaribio la mapinduzi ya kiuchumi dhidi ya nchi yake.

Akizungumza mbele ya hadhara ya chama chake tawala cha AKP mjini Ankara, Jumamosi, kiongozi huyo wa Uturuki alisema baadhi ya watu wanajaribu kutoa vitisho vya kiuchumi dhidi ya nchi yake kupitia riba, fedha za kigeni, uwekezaji na mfumuko wa bei.

Sarafu ya Uturuki, Lira, imepoteza asilimia 30 ya thamani yake mkabala wa dola ya Marekani tokea mwanzo wa mwezi Agosti wakati kuliibuka msuguano baina ya nchi hiyo na Marekani. Nchi hizo mbili washirika katika muungano wa NATO zinazozana baada ya Uturuki kumkamata Andrew Brunson, mhubiri wa Kikristo kutoka Marekani ambaye anakabiliwa na tuhuma za kujihusisha na makundi ya kigaidi.

 

Andrew Brunson

Brunson anakabiliwa na mashtaka ya kuwa na uhusiano na kundi la wanamgambo la PKK ambalo linapigana kujitenga na Uturuki. Aidha anakabiliwa na tuhuma za kuwa na uhusiano na mpinzani Fethullah Gulen anayeishi uhamishoni Markeani na ambaye Uturuki inasema alisimamia njama ya kutaka kuipindua serikali ya Erdogan Julai 2016. Iwapo atapatikana na hatia, atafungwa hadi miaka 35 gerezani. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa mhubiri huyo ni afisa wa ngazi za juu katika Shirika Kuu la Kijasusu la Marekani, CIA.