Erdoğan: Uturuki itayashinda matatizo ya kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48265-erdoğan_uturuki_itayashinda_matatizo_ya_kiuchumi
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa nchi yake inaweza kuyashinda matatizo ya kiuchumi yanayoikabili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2018 10:34 UTC
  • Recep Tayyip Erdoğan
    Recep Tayyip Erdoğan

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa nchi yake inaweza kuyashinda matatizo ya kiuchumi yanayoikabili.

Rais Erdoğan ameyasema hayo akiwahutubia wafanyabiashara wa Kimarekani nchini Uturuki na kufafanua kuwa, ni kosa kubwa kuyaoanisha masuala ya kisiasa na masuala ya kibiashara. Rais wa Uturuki amesema kuwa, ushirikiano wa kistratijia pamoja na Marekani kupitia uwekezaji na biashara utaendelea. Ameongeza kwamba, hapendelei kuona masuala hasi yanayoibuliwa na serikali ya sasa ya Marekani yakiathiri sekta ya biashara ya nchi yake.

Lira, fedha ya Uturuki iliyopoteza thamani yake

Uhusiano wa Uturuki na Marekani ulivurugika tangu kulipojiri mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli mwezi Julai 2016 na baada ya hapo kutiwa mbaroni na serikali ya Ankara padri jasusi wa Kimarekani na hatua ya Washington ya kuwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Uturuki. Kufuatia hayo, sarafu ya Uturuki (Lira) imepoteza thamani yake kwa asilimia 40 mkabala wa Dola ya Marekani.

Hivi karibuni Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki aliwataka raia wa nchi hiyo kutoa akiba zao za fedha za kigeni na kuzibadili kwa fedha ya Lira, sambamba na kuiamini sarafu hiyo ili kuinua tena thamani yake mkabala na Dola ya Kimarekani.