Erdogan: Tutaendelea kununua gesi ya Iran licha ya vitisho vya Trump
Rais Recep Tayyip Erdoğan amesema Uturuki itaendelea kununua gesi kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya vikwazo na vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani.
Katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, Erdoğan amesema, "Tutazame mambo kwa uhalisia wake, je ninapaswa kuwaacha Waturuki waumie na baridi msimu wa kipupwe? Nyumba zao zitapataje joto iwapo tutaacha kununua gesi kutoka Iran?"
Amesema Uturuki inategemea nishati kutoka nchi za nje kwa asilimia 100, na kwamba asilimia 40 ya nishati ya umeme nchini humo inatokana na gesi asilia.
Hapo jana katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Uturuki aliikosoa vikali Marekani kwa kutumia vikwazo kama silaha dhidi ya nchi nyingine.
Uhusiano wa Uturuki na Marekani ulivurugika tangu kulipojiri mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli mwezi Julai 2016 na baada ya hapo kutiwa mbaroni na serikali ya Ankara padri jasusi wa Kimarekani na hatua ya Washington ya kuwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Uturuki.
Marekani imetishia kuziwekea vikwazo nchi zitakazonunua mafuta na gesi kutoka Iran kuanzia Novemba 4.