Trump: Mauaji ya Khashoggi hayatatufanya tufute mauzo ya silaha kwa Saudia
Rais Donald Trump wa Marekani amesema Washington haiwezi kujiweka katika hatari ya kupoteza mabilioni ya dola kutokana na 'madai ya kuuawa' Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mpinzani mkubwa wa utawala wa Aal-Saud, katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki siku chache zilizopita.
Akiongea na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House jana Alkhamisi, Trump alisema, "Je, tufute mauzo hayo kwa maslahi gani? Haya yalifanyika Uturuki na ninavyojua, Khashoggi sio raia wa Marekani."
Jamal Khashoggi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul takriban wiki moja iliyopita.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini Uturuki vimetangaza kwamba, Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi huo mdogo wa Saudia na kisha mwili wake kutupwa nje ya jengo la ubalozi huo.
Kufuatia mauaji hayo, Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani, Rand Paul, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Saudia itaendelea kuwaua raia na waandishi wa habari, madhali sisi (Marekani) tutaendelea kuwauzia silaha. Rais (Trump) anapaswa kusitisha mara moja mauzo ya silaha na uungaji mkono wa kijeshi kwa Saudi Arabia.
Itakumbukwa kuwa akiwa mjini Riyadh mwaka jana wa 2017 katika safari yake ya kwanza nje ya nchi baada ya kuapishwa, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa, Saudi Arabia itanunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 110 kutoka Marekani.