Trump: Marekani kutoiuzia Saudia silaha ni sawa na kujiadhibu
Rais Donald Trump amesema Marekani itakuwa inajiadhibu yenye iwapo itaamua kusimamisha uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia, huku Washington ikiendelea kukabiliwa na mashinikizo ya kuangalia upya uhusiano wake na Riyadh kufuatia mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal-Saud.
Akihutubia waandishi wa habari jana Jumamosi katika Ikulu ya White House, Trump amesema kuna hatua nyingine ambazo Marekani inaweza kuichukulia Saudia badala ya kuacha kuizia silaha.
Amesema iwapo itathibiti kuwa Saudia imemuua Khashoggi, Marekani itaichukulia hatua kali, ingawaje hajaainisha hatua hizo, lakini amesisitiza kuwa kutoiuzia silaha sio moja ya machaguo hayo.
Rais wa Marekani amesema, "Iwapo hawatanunua silaha kutoka kwetu, basi watanunua kutoka Russia na China, tutakuwa wapumbavu sana iwapo tutapoteza dola bilioni 110, na badala yake nchi nyingine zistafidi nazo."
Siku chache zilizopita, Trump alisema Washington haiwezi kujiweka katika hatari ya kupoteza mabilioni ya dola kutokana na 'madai ya kuuawa' Jamal Khashoggi, akisisitiza kwamba tukio hilo lilifanyika Uturuki na Khashoggi sio raia wa Marekani.
Itakumbukwa kuwa akiwa mjini Riyadh mwaka jana wa 2017 katika safari yake ya kwanza nje ya nchi baada ya kuapishwa, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa, Saudi Arabia itanunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 110 kutoka Marekani.