Trump atishia tena kuziwekea ushuru zaidi bidhaa za China
Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kwamba iwapo hakutofikiwa mwafaka na China, basi ataziwekea ushuru mwingine wa mamia ya mabilioni ya Dola, bidhaa za China zinazoingizwa nchi hiyo.
Trump ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya Fox News ambapo ametangaza kiwango cha Dola bilioni 267 cha ushuru tarajiwa dhidi ya bidhaa za China. Hii ni katika hali ambayo, Jumatatu ya jana kanali ya televisheni ya Bloomberg iliripoti kwamba iwapo mazungumzo kati ya China na Marekani hayatokuwa na natija, basi serikali ya Washington itaziwekea ushuru wa forodha bidhaa nyingine za China mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu. Hadi sasa Marekani imekwishaziwekea bidhaa za China ushuru wa thamani ya Dola bilioni 250, huku serikali ya China na katika hatua ya ulipizaji kisasi ikiwa imeziwekea ushuru wa kiasi cha Dola bilioni 110 bidhaa za Marekani zinazoingizwa nchi hiyo ya Asia.
Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China viliibuka kufuatia maamuzi ya Rais Donald Trump ya kuzipandishia ushuru wa forodha bidhaa za aluminiamu na chuma za nchi hiyo kuanzia tarehe nane Machi mwaka huu. Hatua ya Trump ya hivi karibuni katika kuzipandishia ushuru bidhaa za nchi washirika wa kibiashara wa Washington, imekabiliwa na radiamali hasi ya dunia ambapo Umoja wa Ulaya EU na China zimetangaza kwamba, hatua hiyo itapata jibu.