Ujerumani yakosoa uamuzi wa Marekani wa kujitoa katika makubaliano ya INF
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amekosoa uamuzi wa Marekani wa kujitoa katika Makubaliano ya Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) na kuyataja makubaliano hayo kuwa miongoni mwa mikataba muhimu sana ya kudhibiti silaha za nyuklia.
Heiko Mass amesisitiza kuwa makubaliano ya INF yanaiweka mbali dunia na mashindano mengine ya silaha. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amependekeza kuwa Marekani, Ulaya na Russia zipitie upya makubaliano ya silaha yaliyofikiwa hadi sasa na kisha silaha mpya ziongezwe kwenye makubaliano hayo na ziasisi mfumo mpya wa kudhibiti silaha.
Akiendelea kupuuza uwajibikaji katika uga wa kimataifa, Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 20 mwezi huu alitangaza kuwa nchi hiyo inajiandaa kujitoa katika makubaliano ya silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF). Makubaliano ya pande mbili kwa jina la Makubaliano ya Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) yalisainiwa mwaka 1987 na viongozi wa wakati huo wa Marekani na Umoja wa Kisovieti na makubaliano hayo yalitambuliwa kama hatua muhimu katika kuondoa hali ya mivutano katika kipindi cha Vita Baridi.