Donald Trump; rais mbaguzi zaidi katika historia ya Marekani
Mwananadharia na mhadhiri mashuhuri wa taaluma ya siasa katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani amesema kuwa Doland Trump, ndiye rais mbaguzi zaidi wa rangi katika historia ya nchi hiyo.
Akizungumza hivi karibuni, Francis Fukuyama amesema kuwa Rais Donald Trump anawachochea wabaguzi wa rangi wa mrengo wa kushoto kuendelea kuwa na misimamo ya kupindukia mipaka na ya ubaguzi dhidi ya jamii nyingine za nchi hiyo. Fukuyama amesema hatua hizo za Trump ni za makusudi kwa sababu hataki kuwa na mpinzani mwenye nguvu katika uchaguzi mkuu ujao wa 2020. Francis Fukuyama ameendelea kufafanua kwamba hata kama kumekuweko na mgawanyiko katika jamii ya Marekani lakini Trump amegeuka kuwa nembo ya kuchochea mgawanyiko huo kati ya mirengo miwili hasimu ya kulia na kushoto.
Amesema Trump alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 kutokana na uungaji mkono wa wachache na kwa msaada wa mfumo wa uchaguzi wa Marekani. Francis Fukuyama amesema mara tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo, Trump badala ya kufanya juhudi za kurudisha utulivu katika jamii ya Marekani amekuwa akitumia kila fursa kwa ajili ya kuwasha moto wa mgawanyiko nchini humo. Amri, matamshi, hatua na tabia za kutatanisha na mara nyingine za dharau za Donald Trump, zimewapelekea wanasiasa wengi nchini Marekani kusema kuwa rais huyo hafai kuhudumu katika nafasi hiyo.