Watu sita watiwa mbaroni Ufaransa kwa kujaribu kumshambulia Rais Emmanuel Macron
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49343-watu_sita_watiwa_mbaroni_ufaransa_kwa_kujaribu_kumshambulia_rais_emmanuel_macron
Vyombo vya habari nchini Ufaransa vimetangaza kwamba watu sita wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kupanga shambulizi dhidi ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2018 04:07 UTC
  • Watu sita watiwa mbaroni Ufaransa kwa kujaribu kumshambulia Rais Emmanuel Macron

Vyombo vya habari nchini Ufaransa vimetangaza kwamba watu sita wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kupanga shambulizi dhidi ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa habari hiyo, polisi ya Ufaransa imewatia nguvu watu hao kwa kula njama za kumshambulia rais huyo. Hata hivyo polisi hiyo imesema kuwa mpango wa shambulizi hilo ulikuwa haujatimia na kwamba watu hao wanaoshikiliwa ni wanaume watano na mwanamke mmoja ambao wote wana umri wa kati ya miaka 22 na 62.

Polisi ya Ufaransa

Viongozi wa usalama nchini Ufaransa hawajaweka wazi utambulisho wa watu hao. Kutiwa mbaroni kwa watu hao kwa tuhuma za kutaka kumshambulia Rais Emmanuel Macron kumejiri katika hali ambayo mvuto wa rais huyo hususan kwa wafuasi wa mirengo ya kisoshalisti na hata kwa wafuasi wa chama cha Republican umepungua kwa kiasi kikubwa. Kuendelea mwenendo wa ukosefu wa ajira na kushindwa kudhibitiwa hali hiyo ambayo inatajwa na Wafaransa kuwa inayotia wasi wasi mkubwa na kadhalika mdororo wa uchumi na kuongezeka ughali wa maisha ni masuala muhimu yanayowafanya raia wa nchi hiyo kumchukia Rais Emmanuel Macron.