Mwanamke auawa katika maandamano ya kulalamikia ughali wa mafuta Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49591-mwanamke_auawa_katika_maandamano_ya_kulalamikia_ughali_wa_mafuta_ufaransa
Mwanamke mmoja ameuawa katika maandamano makubwa ya kulalamikia ughali wa mafuta ya petroli kote Ufaransa siku ya Jumamosi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2018 03:41 UTC
  • Mwanamke auawa katika maandamano ya kulalamikia ughali wa mafuta Ufaransa

Mwanamke mmoja ameuawa katika maandamano makubwa ya kulalamikia ughali wa mafuta ya petroli kote Ufaransa siku ya Jumamosi.

Kwa mujibu wa taarifa, makumi ya maelfu ya watu walijitokeza kote Ufaransa kulalamikia ughali wa maisha hasa ongezeko kubwa la mafuta ya petroli. Inakadiriwa kuwa karibu waandamanaji 240,000 walijitokeza katika maeneo mbali mbali ya Ufaransa ambapo walifunga barabara kuu huku wakikabiliana na polisi wa kuzima ghasia. Msongamano mkubwa wa magari ulisuhuhudiwa katika maeneo mengi hasa katika mji mkuu Paris.

Baadhi ya waandamanaji mjini Paris walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa 'Macron Jiuzulu' huku wakiimba wimbo wa taifa katika eneo la Champs Elysees katikati mwa mji huo mkuu wa Ufaransa.

Wananchi wanalalamikia sera za marekebisho ya kiuchumi za Rais Macron wa Ufaransa hasa uamuzi wa kuongeza ushuru wa petroli jambo ambalo limeongeza ughali wa maisha katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Rais Macron wa Ufaransa

Waandamanaji wanataka viwanda vikubwa na matajiri Ufaransa wabebe mzigo wa ushuru badala ya serikali kuongeza bei ya mafuta ambayo itamuumiza mwananchi wa kawaida.

Hali mbaya ya maisha imepelekea umashuhuri wa Macron kushuika kutoka asilimia 39 mwezi Julai hadi asilimia 21 mwezi Oktoba.