Washington Post: Mchakato wa kifo cha kisiasa cha Donald Trump umeanza
Gazeti la Washington Post limeandika makala ya ripoti ya kuchunguza siasa za vituko za rais Donald Trump wa Marekani na kile lilichokieleza kama kifo cha kisiasa cha kiongozi huyo.
Katika ripoti yake hiyo, Washington Post limeandika kuwa, wakati hasa wa kutokea kifo cha kisiasa cha Donald Trump haujulikani, lakini mchakato huo umeanza wakati wa uchaguzi wa mwaka huu wa Bunge, ambapo idadi tosha ya Wamarekani walifikia natija kwamba Trump ameshafanya uharibifu kwa kiwango cha kutosha.
Kwa ujumla, mjibizo na radiamali ya Trump yenye hisia za ubaguzi wa rangi wakati wa tukio la Charlottesville, kukwamisha kutekelezwa uadilifu, kutishia kukata misaada ya serikali kuu kwa raia wa jimbo la California walioathiriwa na maafa au utumiaji mbaya mwengine wowote wa mamlaka ya utendaji, unatajwa kama sababu ya kifo cha kisiasa cha kiongozi huyo.
Washington Post aidha limeandika, jumbe za Twitter za lugha chafu ya ukosoaji, utani wa kipumbavu aliofanya hivi karibuni kuhusu jina la mbunge mmoja wa Kongresi ya Marekani na mienendo yake isiyokubalika kama kuamini maelezo ya dola ajinabi badala ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo nchini Uturuki, yote hayo ni mambo yatakayoendelea kushuhudiwa.
Kwa mujibu wa Washington Post, Trump hatatolewa ghafla nje ya siasa za Marekani kwa sababu ya jambo moja tu litakalodhihirika wazi lakini uhai wake wa kisiasa utafikia kikomo kwa sababu ya mchanganyiko wa mienendo yake ambayo ni ya kujidhuru mwenyewe.../