Mbunge wa Marekani: Trump ni kijakazi cha Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49685-mbunge_wa_marekani_trump_ni_kijakazi_cha_saudia
Mbunge wa Kongresi ya Marekani amemtaja rais wa nchi hiyo, Donald Trump kuwa ni kama kijakazi cha Saudi Arabia, kutokana na misimamo ya kuukingia kifua na kuutetea utawala wa Aal Saud.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 22, 2018 11:22 UTC
  • Mbunge wa Marekani: Trump ni kijakazi cha Saudia

Mbunge wa Kongresi ya Marekani amemtaja rais wa nchi hiyo, Donald Trump kuwa ni kama kijakazi cha Saudi Arabia, kutokana na misimamo ya kuukingia kifua na kuutetea utawala wa Aal Saud.

Tulsi Gabbard wa wilaya ya D-Hawaii amesema, misimamo hiyo ya Trump inakinzana na mambo aliyoyaahidi katika kampeni za uchaguzi wa rais. Ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Kuwa kijakazi cha Saudia sio sera ya 'Marekani Kwanza' aliyoitangaza Trump wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais.

Ameongeza kuwa, inashangaza kuiona Marekani inaendelea kusimama na Saudia licha ya ripoti ya CIA kufichua nafasi ya watala wa Riyadh katika mauaji ya Khashoggi.

Siku chache zilizopita, duru za kuaminika zililiambia gazeti la Washington Post kwamba, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limefikia natija kwamba, Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa Jamal Khashoggi ambaye alikuwa mkosoaji wa utawala wa Aal Saud. 

Kwa mujibu wa CIA, Mrithi wa Kiti cha Ufalme Saudia ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa Khashoggi

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House siku Jumanne, Trump alisema, "Kuna uwezekano Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman alikuwa na taarifa ya mpango wa kuuliwa Khashoggi, lakini hata hivyo uhusiano wetu na utawala wa Saudia utazidi kuwa imara, kwani ni washirika wetu wakubwa katika vita vyetu muhimu dhidi ya Iran. Tutaendelea kushirikiana nao, kwa maslahi yetu, na kwa maslahi ya Israel na waitifaki wetu wengine katika eneo."

Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, aliuliwa kikatili kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Uturuki, tarehe Pili mwezi uliopita wa Oktoba.