Nusu ya Wafaransa hawakuridhishwa na ahadi za Rais wa nchi hiyo
Nusu ya wananchi wa Ufaransa hawakuridhishwa na hotuba iliyotolewa na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo aliyekuwa katika jitihada za kutuliza ghasia na machafuko makubwa ya Wafaransa wanaopinga ughali wa maisha na sera za kiuchumi za serikali ya sasa ya Paris.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya OpinionWay yanaonesha kuwa, hotuba iliyotolewa jana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa haikuwakinaisha asilimia isiyopungua 50 ya Wafaransa. Robo ya walioshiriki katika uchunguzi huo wa maoni wanasema Macron hakutoa jibu lolote kuhusu malalamiko ya wapinzani wa sera na siasa zake za kiuchumi.
Vilevile asilimia 45 ya washiriki katika uchunguzi huo wa maoni wameunga mkono suala la kuendelezwa maandamano dhidi ya serikali ya Ufaransa.
Katika hotuba yake ya jana usiku, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliwaahidi Wafaransa kwamba, atatumia njia zote kurejesha amani na utulivu nchini humo. Amesema kuwa serikali yake itapunguza ushuru haraka iwezekanavyo, kubana matumizi ya umma na kushughulikia matatizo ya kijamii na kiuchumi.
Wafaransa wamekuwa wakiandamana dhidi ya ughali wa maisha, ongezeko la bei ya mafuta ya petroli na sera za kibepari. Waandamanaji wanataka Rais Emmanuel Macron aondoke madarakani kutokana na hali mbaya inayosuhudiwa nchini humo.
Polisi ya Ufaransa imetumia gesi ya kutoa machozi, mabomu ya sauti na mipira ya maji kwa ajili ya kutawanya maelfu ya raia wa nchi hiyo wanaoandamana katika miji mbalimbali hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo, Paris na watu zaidi ya 1400 wametiwa nguvuni.
Maandamano hayo yaliyoanzishwa na kundi la watu wanaojiita harakati ya wavaaji wa "vizibao vya njano", yanapinga ongezeko la bei ya fueli ya dizeli inayotumiwa zaidi katika magari nchini Ufaransa na kupanda juu gharama za maisha.