Macron: Maandamano ya vizibao vya njano yasitishwe
Sambamba na kuanza wimbi jipya la maandamano ya harakati iliyopata umaarufu kwa jina la Vizibao vya Njano nchini Ufaransa; Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ametaka kusitishwa maandamano hayo na kurejeshwa hali ya utulivu nchini humo.
Rais Macron alitangaza jana kuwa wakati umefika sasa wa kurejesha amani, utulivu na uratibu nchini humo na kutatua hitilafu zilizopo. Ripoti za karibuni zinaonyesha kuwa polisi ya Ufaransa imewatia mbaroni watu wasiopungua 220 tangu juzi Jumamosi sambamba na kuanza duru hiyo mpya ya maandamano nchini humo.
Ghasia za karibuni nchini Ufaransa za kulalamikia siasa za kiuchumi za serikali ya nchi hiyo zilianza tarehe 17 mwezi Novemba mwaka huu; na hivi sasa ghasia hizo zimeenea pia katika nchi nyingine za Ulaya ikiwemo Uholanzi na Ubelgiji. Hatua ya polisi ya Ufaransa ya kutumia mabavu kukabiliana na maandamano hayo ya Vizibao vya Njano hadi sasa imesababisha vifo vya watu 10, majeruhi kadhaa na mamia kutiwa nguvuni.