Vizibao vya njano na kuendelea siku ngumu zinazomkabili Macron nchini Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50392-vizibao_vya_njano_na_kuendelea_siku_ngumu_zinazomkabili_macron_nchini_ufaransa
Sambamba na kuanza wimbi jipya la maandamano ya harakati iliyopata umaarufu kwa jina la "Vizibao vya Njao" nchini Ufaransa, Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ametaka kusimamishwa mwenenendo huo na kurejeshwa utulivu nchini humo. Macron amesema kuwa umefika wakati sasa wa kurejeshwa amani, utulivu na mambo kurejea katika hali yake ya kawaida nchini humo na kutatuliwa hitilafu zilizopo.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Dec 24, 2018 08:27 UTC
  • Vizibao vya njano na kuendelea siku ngumu zinazomkabili Macron nchini Ufaransa

Sambamba na kuanza wimbi jipya la maandamano ya harakati iliyopata umaarufu kwa jina la "Vizibao vya Njao" nchini Ufaransa, Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ametaka kusimamishwa mwenenendo huo na kurejeshwa utulivu nchini humo. Macron amesema kuwa umefika wakati sasa wa kurejeshwa amani, utulivu na mambo kurejea katika hali yake ya kawaida nchini humo na kutatuliwa hitilafu zilizopo.

Rais Macron anaonekana kuchukua msimamo huo katika hali ambayo hivi sasa harakati hiyo ya vizibao vya njano si tu imetaka kutekekelezwa matakwa yao ya kiuchumi na kisiasa, bali pia inalalamikia utumiaji mabavu na hatua zisizo za kidemokrasia za polisi wa nchi hiyo katika kuamiliana na waandamanaji. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Mgogoro wa maandamano ya wanaharakati wa vizibao vya njano umekuwa mkubwa zaidi huko Ufaransa na hatua ya polisi ya kuamiliana kwa mabavu na wafanya maandamano imewakasirisha sana wanaharakati hao. Hata kama duru ya sita ya maandamano haya imekuwa ya kasi ya chini ikilinganishwa na wiki kadhaa zilizopita, lakini filamu iliyooneshwa katika televisheni mbalimbali ambapo ndani yake inamuonyesha polisi mmoja akiburuta silaha yake juu ya waandamanaji katika mtaa wa Champs Elysees (Chanze Lize) katika mji mkuu Paris imeibua wimbi jipya la malalamiko.   

Kwa mujibu wa taarifa za karibuni, polisi wa Ufaransa katika maandamano ya Jumamosi wiki hii waliwatia mbaroni watu wasiopungua 220. Polisi wa Ufaransa wanatumia nguvu kupita kiasi na kuwakandamiza raia wanaoandamana huku wachambuzi wa mambo wakikitaja kiwango hicho cha ukandamizaji wa polisi wa Ufaransa dhidi ya waandamanaji kuwa ni cha aina yake kuwahi kushuhudiwa kwenye muda mfupi wa mwezi mmoja katika historia nzima ya Ufaransa. Vyombo vya mahakama vya Ufaransa vimetangaza kuwa hivi sasa vinashughulikia kesi 36 zinazohusiana na vitendo vya utumiaji mabavu pakubwa vya polisi wa nchi hiyo dhidi ya wanafunzi wa shule ya msingi waliokuwa wakiandamana na wanaharakati wanaopinga mfumo wa ubepari nchini humo.   

Ahmad Muumini-Rad mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na kadhia hii kwamba: Serikali ya Ufaransa ambayo inajinadi kuwa mtetezi wa haki za binadamu na ambayo inalalamikia hatua zinazochukuliwa na nchi nyingine; hii leo yenyewe inakabiliana kwa ukandamizaji na kutumia mabavu vikali na wananchi wanaoandamana nchini humo. Ni wazi kuwa hii leo nchi za Magharibi zinatumia kama wenzo suala la haki za binadamu na demokrasia ili kufanikisha malengo yao zilizoyakusudia katika nchi nyingine. 

Maandamano ya harakati ya vizibao vya njano huko Ufaransa hivi sasa yameingia katika wiki yake ya saba ambapo rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron alikuwa akitaraji kwamba angefanikiwa kupunguza ghadhabu na hasira za waandamanaji kutokana na ahadi alizotoa na hivyo maandamano hayo kusitishwa. Rais Macron aidha ameonekana kulegeza msimamo wake kuhusu uamuzi kama wa kuongeza kodi ya mafuta ya dizeli, na hivyo akatoa ahadi ya kuongeza mishahara na marupurupu na kuzingatia zaidi hali ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa Ufaransa. Hata hivyo licha ya ahadi zote hizo za Rais wa Ufaransa, wafanya maandamano nchini humo hivi sasa si tu kuwa wanafuatilia matakwa yao ya kiuchumi lakini pia wanataka Rais Macron ajiuzulu.  

Edouard Philippe, Waziri Mkuu wa Ufaransa 

Wafanya maandamano hao wanamtambua Macron kuwa ni Rais tajiri na wanaamini kwamba siasa za kiuchumi za rais huyo na kutotilia maanani matakwa ya wananchi wake ndiyo chanzo cha kushuhudiwa matatizo ya kiuchumi na kuenea dhulma na uonevu nchini Ufaransa.  

Edouard Philippe Waziri Mkuu wa Ufaransa anazungumzia kadhia hiyo akisema: Serikali ya Ufaransa imekosea katika kudhibiti maandamanano ya wanaharakati wanaopinga ubapari nchini humo na haijatilia maanani vya kutosha matakwa ya wananchi wake.  

Pamoja na hayo yote, Rais Macron kwa mara nyingine tena amesisitiza kurejeshwa hali ya utulivu huko Ufaransa na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote watakaovunja sheria. 

Katika kukaribia mwaka mpya wa Milaadia, wafanya maandamano nchini humo wamesema: "Sisi hatuna Noel; Noel ni ya matajiri kwa asilimia mia moja."

Katika mazingira kama haya inaonekana kuwa ahadi na hata vitisho vilivyotolewa na Rais wa Ufaransa haviwezi kuisimamisha harakati ya Vizibao vya Njano. Kwa msingi huo inatarajiwa kwamba katika sikukuu hizi za mwaka mpya, Ufaransa itagubikwa pia na  ghasia na machafuko.