Wafaransa waunga mkono harakati dhidi ya mfumo wa ubepari
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50768-wafaransa_waunga_mkono_harakati_dhidi_ya_mfumo_wa_ubepari
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Ufaransa yanaonyesha kuwa akthari ya wananchi wa nchi hiyo wanaunga mkono harakati inayopinga mfumo wa ubepari.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jan 10, 2019 03:56 UTC
  • Wafaransa waunga mkono harakati dhidi ya mfumo wa ubepari

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Ufaransa yanaonyesha kuwa akthari ya wananchi wa nchi hiyo wanaunga mkono harakati inayopinga mfumo wa ubepari.

Uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na taasisi ya Elabe unaonyesha kuwa asilimia 60 ya wananchi wa Ufaransa wanaendelea kuiunga mkono harakati hiyo iliyo dhidi ya mfumo wa ubepari. Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, asilimia 51 ya Wafaransa wanaamini kuwa, harakati hiyo inayoipinga serikali ya Rais Emmanuel Macron, inapasa kuendelea na shughuli zake. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa 

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yamebainisha kuwa asilimia 78 ya wananchi wa Ufaransa pia wanaalani ghasia na utumiaji mabavu vilivyoshuhudiwa katika maandamano ya harakati hiyo liyopewa jina la "Vizibao vya Njano".

Wakati huo huo serikali ya Ufaransa imetangaza kuwa itakabiliana vikali na maandamano ya Jumamosi ijayo ya tarehe 12 mwezi huu. 

Harakati ya Vizibao vya Njano ilianza maandamano makubwa ya nchi nzima Novemba 17 mwaka jana kulalamikia hatua ya serikali ya Ufaransa ya kuongeza kodi ya nishati na tangu wakati huo maandamano hayo yamekuwa yakifanyika kila siku ya Jumamosi  licha ya kukabiliwa na ukandamizaji wa polisi. Watu kumi wameuawa, 5,600 wamefungwa jela na maelfu wamejeruhiwa tangu kuanza maandamano hayo ya Vizibao vya Njano nchini Ufaransa.