Maandamano ya harakati ya Vizibao vya Njano yaanza tena Ufaransa
Wananchi wa Ufaransa wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakiendelea kupinga mfumo wa ubepari na sera za kiuchumi za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.
Harakati hiyo ya Vizibao vya Njano kwa mara nyingine tena leo Jumamosi imefanya maandamano katika Jumamosi ya tisa mtawalia ikipinga mfumo wa ubepari nchini Ufaransa. Ripoti zinasema kuwa wafanya maandamano katika eneo la Bastille katika mji mkuu, Paris walikuwa wakipiga nara dhidi ya Rais Emmanuel Macron. Maandamano mengine kama hayo yameripotiwa katika mji wa Lyon nchini Ufaransa.
Watu karibu elfu 50 wiki iliyopita waliandamana katika miji mbalimbali ya Ufaransa kuunga mkono harakati ya Vizibao vya Njano. Harakati hiyo ilianza kufanya maandamano tarehe 17 mwezi Novemba mwaka jana kupinga mipango ya kiuchumi inayotekelezwa na serikali ya Ufaransa ikiwemo hatua ya kupandisha kodi ya nishati. Hadi sasa polisi ya Ufaransa imethibitisha kuuawa watu kumi kwenye maandamano hayo.