Mbunge Mwislamu wa Marekani ataka Washington isiiuzie silaha Saudia
-
Ilhan Omar
Mbunge wa kwanza mwanamke Mwislamu katika Kongresi ya Marekani ametoa wito wa kusitishwa uuzaji wa silaha kwa utawala wa Saudi Arabia.
Katika siku ya kwanza ya kazi zake kama mjumbe wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Kongresi ya Marekani, Ilhan Omar ameitaja Saudi Arabia kuwa ni utawala unaokiuka haki za binadamu na kutaka serikali ya Washington isitishe uuzaji wa silaha kwa nchi hiyo.
Kutokana na misimamo yake hiyo imara ya kupinga ukandamizaji unaofanywa na Saudi Arabia, mbunge Ilhan Omar wa Kongresi ya Marekani amekuwa akishambuliwa mara kwa mara na vyombo vya habari vya serikali ya Riyadh. Baada ya mbunge huyo kushinda katika uchaguzi wa bunge uliofanyika tarehe 6 Novemba mwaka 2018, vyombo vya habari vya Saudia vilimtuhumu Ilhan Omar kwamba ni sehemu ya mrengo wa Kiislamu unaotaka kudhibiti Kongresi ya Marekani.
Mashirika na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikitoa wito wa kusitishwa uuzaji wa silaha za nchi hizo kwa utawala wa kiimla wa Saudi Arabia kutokana na mauaji yanayofanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya watu wasio na hatia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo.

Maelfu ya Wayemeni wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya Saudi na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.