Uwezekano wa kutimuliwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani waongezeka
Ripoti mbalimbali kutoka Marekani zinasema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo atatimuliwa kazi kutokana na kushadidi hitilafu ndani ya Ikulu ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Jarida la Marekani la The Politico limefichua kwamba, kuna uwezekano mkubwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo atapigwa kalamu nyekundu na Trump.
Hadi sasa Pompeo hajasema lolote kuhusu suala hilo, japokuwa wajumbe wa chama cha Republican katika Baraza la Seneti la Marekani wamekuwa wakijadili kadhia hiyo.
Pompeo alikuwa mkurugernzi wa shirika la ujasusi la Marekani CIA kabla ya kuteuliwa na Donald Trump kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Kipindi cha uongozi wa Donald Trump nchini Marekani kinatajwa kuwa kilichoshuhudia mivutano mikubwa na mingi zaidi ndani ya Ikulu ya White House na hadi sasa maafisa wengi wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi wa nchi hiyo wamejiuzulu au kutimuliwa kazi kutokana na kuhitilafiana kwao na sera za kimabavu na kibaguzi za kiongozi huyo.