Waziri wa Ulinzi wa Venezuela: Hatumtambui Juan Guaidó kuwa rais
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51082-waziri_wa_ulinzi_wa_venezuela_hatumtambui_juan_guaidó_kuwa_rais
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amesisitiza kwamba, jeshi la nchi hiyo halimuungi mkono Juan Guaidó aliyejitangaza kuwa rais mpya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 24, 2019 04:38 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Venezuela: Hatumtambui Juan Guaidó kuwa rais

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amesisitiza kwamba, jeshi la nchi hiyo halimuungi mkono Juan Guaidó aliyejitangaza kuwa rais mpya.

Vladimir Padrino López, ameyasema hayo baada kiongozi wa upinzani na anayeungwa mkono na Marekani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo na kuongeza kwamba majeshi ya Venezuela yataendelea kulinda usalama na haki ya kujitawala kwa mujibu wa katiba. Kabla ya hapo pia Rais Nicolás Maduro na katika radiamali yake kutokana na uingiliaji wa Marekani na hatua za kiongozi wa upinzani kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo amesema kuwa kamwe hatosalimu amri. Sambamba na kutangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Marekani Rais Maduro amewapa wanadiplomasia wa Marekani masaa 72 wawe wameondoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Rais Nicolás Maduro akiwa na Vladimir Padrino López

Ameongeza kwamba, Marekani inafanya njama kuitwisha Venezuela rais asiye wa kisheria na kwamba kitendo hicho ni kosa kubwa la Washington. Jumatano ya jana Juan Guaido ambaye alitimuliwa katika chama cha Kongresi ya kitaifa alijitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo. Hayo yanajiri huku Marekani na Umoja wa Ulaya sambamba na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo zimetangaza kumuunga mkono Juan Guaido, huku zikiitisha uchaguzi wa mapema.