Viongozi wa Russia wakosoa uingiliaji mambo wa Marekani nchini Venezuela
Viongozi kadhaa wa kisiasa nchini Russia wamekosoa uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kumtambua kiongozi wa chama cha upinzani nchini Venezuela, Juan Guaido kuwa rais wa muda wa nchi hiyo.
Katika uwanja huo, Andrey Klimov naibu mkuu wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Baraza la Federesheni nchini Russia sambamba na kukosoa uamuzi huo wa Trump amesema kuwa Marekani inafanya njama za kuratibu operesheni za kimapinduzi nchini Venezuela. Naye kwa upande wake Vladimir Dzhabirulov, mjumbe mwingine wa kamati hiyo amesema kwamba suala hilo kimsingi ni mapinduzi ya kijeshi dhidi ya nchi iliyo huru.
Jumanne iliyopita Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na bila kuzingatia chaguo la wananchi wa Venezuela waliomchagua Nicolás Maduro, aliingilia wazi wazi masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini na kumtaka aondoke madarakani na kumpisha Juan Guaido, anayeungwa mkono na Wamagharibi. Tayari Juan Guaido amejitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela suala ambalo limelaaniwa vikali na serikali ya Caracas. Katika radiamali yake, Rais Maduro ametoa amri ya kukatwa kikamilifu uhusiano wa nchi yake na Marekani.