EU yaiweka Saudia katika orodha ya wafadhili wa ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51126-eu_yaiweka_saudia_katika_orodha_ya_wafadhili_wa_ugaidi
Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imeiweka Saudi Arabia katika rasimu ya orodha ya nchi zilizoshindwa kupambana na utakatishaji wa fedha chafu na ambazo ni wafadhili wa makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2019 04:40 UTC
  • EU yaiweka Saudia katika orodha ya wafadhili wa ugaidi

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imeiweka Saudi Arabia katika rasimu ya orodha ya nchi zilizoshindwa kupambana na utakatishaji wa fedha chafu na ambazo ni wafadhili wa makundi ya kigaidi.

Vyanzo vya habari vimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kamisheni hiyo ya EU imeiangalia upya orodha hiyo na kuiongeza jina la Saudia. 

Uamuzi huo ni pigo kwa Aal-Saud ambayo kwa sasa ipo katika harakati ya kujaribu kusafisha sura yake kimataifa, baada ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, Oktoba 2 mwaka jana.

Ushahidi na nyaraka zote zilizopo, zikiwemo taarifa zilizotolewa na serikali ya Uturuki na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) zinaonyesha kuwa Muhammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa  mauaji ya Jamal Khashoggi, aliyeuawa kikatili kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki

Shirikisho la Kupambana na Fedha Chafu na Ufadhili wa Makundi ya Kigaidi (FATF)

Septemba mwaka jana, Saudi Arabia ilikataliwa uanachama kamili katika Shirikisho la Kupambana na Fedha Chafu na Ufadhili wa Makundi ya Kigaidi (FATF), ambayo ni bodi ya kimataifa ya kupambana na fedha chafu na ufadhili wa kifedha wa makundi ya kigaidi.

Kwa mujibu wa shirika la FATF, utawala wa Riyadh umeshindwa kukamilisha viwango vinavyohitajika vya kupambana na utakatishaji wa fedha chafu na kufadhili makundi ya kigaidi.