Trump: Kufungwa tena serikali, ni moja ya machaguo yetu
Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa, kufungwa kwa mara nyingine shughuli za serikali, ni miongoni mwa machaguo makuu kwa ajili ya kukabiliana na Kongresi kuhusiana na kadhia ya ujenzi wa ukuta wa mpakani.
Trump ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la The Wall Street Journal ambapo ameonyesha wasi wasi wake juu ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano na wabunge wa kongresi kwa ajili ya kutenga bajeti ya ujenzi wa ukuta wa mpakani na kusema kuwa kufungwa tena shughuli za serikali ni miongoni mwa machaguo ya moja kwa moja juu ya kutatuliwa kadhia hiyo. Trump amefafanua kuwa, iwapo Wademocrat hawatokubali kudhamini bajeti ya ujenzi wa ukuta huo katika mpaka wa Mexico, hatokubaliana na mapendekezo yao mengine.
Kundi la watu 17 kutoka Democrat na Republican ambalo limetakiwa kufuatilia makubaliano kuhusiana na usalama wa mpakani na kadhalika kutatua tofauti zilizopo kati ya White House na Kongresi ya nchi hiyo, litaanza vikao vyake wiki hii. Hii ni katika hali ambayo Trump ameonya kwamba, ikiwa bunge la Kongresi halitotenga bajeti ya ujenzi wa ukuta huo wenye lengo la kuzuia wahajiri haramu kuingia nchini humo, basi atatangaza hali ya hatari sambamba na kujenga ukuta huo kwa bajeti ya jeshi. Tofauti kati ya Trump na bunge hilo, zimepelekea kufungwa kwa robo ya shughuli za serikali ya federali kwa siku 35.