Kukwama mazungumzo ya kibiashara baina ya Marekani na China
Rais wa Marekani, Donald Trump ameendeleza siasa zake za kujikumbizia kila kitu upande wake kwa madai ya kulinda uchumi wa Marekani na kwa mara nyingine ametishia kuziwekea ushuru mpya bidhaa za China zinazoingia nchini humo licha ya kwamba Beijing ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Washington.
Katika mazungumzo baina ya rais wa Marekani, Donald Trump na mwenzake wa China, Xi Jinping, yaliyofanyika pambizoni mwa kikao cha viongozi wa kundi la G20 huko Argentina, nchi hizo mbili zilitangaza usimamishaji vita vya kibiashara kwa muda wa siku 90 baina yao. Baada ya hapo, yaani tarehe 30 na 31 mwezi ulioisha wa Januari 2019, pande hizo mbili zilifanya mazungumzo ya ngazi za juu mjini Washington ambayo yalihudhuriwa pia na Liu He, Naibu Waziri Mkuu wa China kwa shabaha ya kufikia makubaliano ya pande mbili kuhusu biashara. Hata hivyo ripoti zinasema kuwa, mazungumzo hayo yameshindwa kuzaa matunda, bali kwa lugha ya moja kwa moja ni kwamba yamevunjika. Jambo hilo limemfanya Trump atoe vitisho vipya dhidi ya Beijing kama kawaida yake. Kiujumla ni kwamba Marekani imeonesha wazi kuwa haina nia kabisa ya kutatua ugomvi wake na China kwa njia za amani.
Katika mazungumzo yake ya siku ya Alkhamisi na Liu He, Naibu Waziri Mkuu wa China, Donald Trump alidai kuwa kumefikiwa matunda mazuri katika mazungumzo hayo kiasi kwamba hata alisema kuwa ana matumaini ya kufikiwa mapatano na kwamba yuko tayari kuonana ana kwa ana na Rais Xi Jinping wa China. Hata hivyo hapo hapo Trump ametoa vitisho kama ada yake. Amesema: Mapatano ya kusimamisha vita vya kibiashara kwa muda wa siku 90 baina ya Marekani na China ni makataa yanayomalizika siku maalumu na kwamba Marekani itaziongezea ushuru bidhaa za China zinazoingia nchini humo isipokuwa tu kama nchi hizo mbili zitafikia natija ya kuridhisha katika mazungumzo yao. Makataa hayo yanamalizika tarehe 1 Machi, 2019. Kama tunavyoona, matamshi hayo ya Trump yamejaa vitisho na kwa hakika anajaribu kuitishia China kuwa, kama haitokubaliana kikamilifu na matakwa ya Marekani basi itaadhibiwa ikiwa ni pamoja na kuongezewa ushuru bidhaa zake zinazoingia nchini Marekani.
Katika mazungumzo ya pande hizo mbili, Wamarekani wameitaka China iwatekelezee mambo yao mengi. Muhimu zaidi kuliko yote ni pamoja na kudai kuwa Wachina wanaiba taarifa na utaalamu wa China hivyo waache kufanya hivyo. Vile vile ni kuwataka Wachina waondoe vizuizi katika soko na kwenye ushuru na hivyo kuruhusu bidhaa za kilimo na nyinginezo za Marekani ziuzwe kwa uhuru zaidi nchini China n.k. Kwa kweli kuitaka China inunue bidhaa za Marekani, ni sehemu muhimu ya mazungumzo ya pande hizo mbili.
Ingawa rais wa Marekani anadai kuwa ana silaha nyingi za kuilazimisha China itii amri na kutekeleza matakwa ya kibiashara ya Washington, lakini kwa kuzingatia kuwa Marekani ina deni kubwa sana la China linalokadiriwa kufikia dola trilioni mbili, China ndiyo inayoonekana kuwa na silaha kali zaidi ya kuweza kuishinikiza vibaya kiuchumi na kibiashara Marekani. Kiujumla ni kwamba China haikubaliani hata kidogo na siasa za rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump, kwani zinakwenda kinyume kabisa na maslahi ya Beijing.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Bruno Le Maire, kama mivutano ya kibiashara baina ya China na Marekani itabadilika na kuwa vita baridi, basi kuna hatari athari zake mbaya zikaikumba dunia nzima.
Kwa kweli siasa za kibiashara za Trump zitapelekea kupanda kwa bei za bidhaa za China katika masoko ya Marekani na matokeo yake yatakuwa ni kupungua wanunuzi wa bidhaa hizo, suala ambalo litakuwa na taathira kubwa mbaya kwa China. Ijapokuwa Wachina wanafanya juhudi mbalimbali za kulinda biashara yao na Marekani, lakini kama Trump hana nia njema, bila ya shaka yoyote China nayo itasimama kidete kukabiliana na tamaa kubwa kupindukia ya rais huyo wa Marekani.