Utafiti: Akthari ya Wamarekani wanasema nchi inaelekea pabaya
Utafiti mpya wa maoni unaonesha kuwa aghalabu ya wananchi wa Marekani wanahisi kuwa nchi yao iko katika mkondo mbaya, huku wengi wao wakikata tamaa.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la habari la Associated Press kwa ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Umma cha NORC umebainisha kuwa, asilimia 70 ya Wamarekani wanahisi kuwa taifa lao linaelekea pabaya, huku asilimia 28 pekee wakiwa na matumaini ya mustakabali mzuri.
Kiwango hicho cha Wamarekani kupoteza matumaini kinatajwa kuwa kikubwa zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Kiwango hicho kilikuwa asilimia 59 mwezi Disemba mwaka uliomalizika.
Asilimia 52 ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo wanasema mambo yatakuwa mabaya zaidi mwaka huu 2019, huku aghalabu yao wakionesha kutamaushwa na hali ya mambo.
Kadhalika utafiti huo wa shirika la habari la Associated Press kwa ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Umma cha NORC umebainisha kuwa, asilimia 34 tu ya wananchi wa Marekani ndio wanaounga mkono namna Rais Donald Trump anavyoendesha nchi.
Utafiti wa maoni wa wiki jana wa shirika la habari la ABC News pamoja na gazeti la Washington Post ulisema kuwa karibu nusu ya Wamarekani (asilimia 48) hawana imani na Trump.