Maveterani wa UK: Tuliamrishwa tuwaue kwa kuwapiga risasi raia Iraq, Afghanistan
Jeshi la Uingereza liliwaagiza askari wake wawaue kwa kuwafyatulia risasi raia wa Iraq na Afghanistan hata kama hawakuwa wamejizatiti kwa silaha.
Katika mahojiano ya kipekee na shirika la habari la Middle East Eye, maveterani hao wa Uingereza wamekiri kuwa waliua hata watoto wadogo katika operesheni zao katika nchi hizo za Kiislamu, na kisha kuweka silaha pambizoni mwa maiti zao ili kupotosha ukweli wa mambo.
Mmoja wa askari hao wastaafu wa Uingereza amefichua kuwa, mwaka 2007 katika mji wa Basra nchini Iraq, walipewa maagizo ya kumfyatulia risasi na kumua raia yeyote watakayemuona akiwa amebeba hata simu ya mkononi, na wakahisi kuwa ni hatari kwao.
Amesema, "Tulikuwa tunawafyatulia risasi wazee na vijana licha ya kuwa hawakuwa na silaha. Sijawahi kuona ukiukaji wa sheria wa kiwango hicho. Hayo ndiyo niliyoyashuhudia binafsi."
Askari mwingine wa Uingereza amefichua namna alivyomuua kwa kumfyatulia risasi mtoto wa miaka minane hivi nchini Afghanistan, na akalazimika kukiri kuwa ndiye aliyefanya ukatili huo, baada ya baba ya mtoto huyo kwenda katika kambi ya jeshi hilo vamizi huku akiwa amenyanyua juu kichwa cha mtoto wake huyo, akitaka kufafanuliwa sababu za kuuawa mwanawe.
Maveterani hao wamesema, "Makamanda wetu walituambia kuwa wangetulinda iwapo uchunguzi wa wimbi la mauaji dhidi ya raia katika nchi hizo za Iraq na Afghanistan ungeanzishwa."
Mwanajeshi mmoja wa Uingereza aliyehudumu katika kambi ya jeshi ya Nad-e Ali mjini Helmand nchini Afghanistan mwaka 2010, ameliambia shirika la habari la Middle East Eye kuwa, aliwafyatulia risasi 12 vijana wawili walioonekana wakitembea kwenda upande wa kituo hicho cha kijeshi cha Uingereza, na mauaji hayo yakafichwa na makamanda wake.
Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Magharibi zimezivamia nchi kadhaa za Waislamu kama vile Syria, Iraq na Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuua mamia ya maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hizo.