Michael Cohen: Trump ni mbaguzi wa rangi, tapeli na mdanganyifu
Aliyekuwa wakili wa rais wa Marekani Donald Trump amesema, kiongozi huyo ni mbaguzi wa rangi, tapeli na mdanganyifu; na yeye anajuta kufanya kazi naye.
Michael Cohen aliyasema hayo katika utangulizi wa maelezo yake aliyotoa wakati alipofika mbele ya kamati ya Baraza la Wawakilishi la Marekani kutoa ushahidi wake wa mwisho kabla ya kupelekwa jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa kadhaa yanayohusiana na ukwepaji kodi na matumizi ya fedha za kampeni ya uchaguzi wa rais.
Kabla ya Cohen kutoa maelezo yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Mageuzi ya Baraza la Wawakilishi la Marekani, Elijah Cummings alimtanabahisha wakili huyo wa zamani wa Trump kuwa "siku za kumkingia kifua rais kwa gharama zozote zile, zimekwisha."
"Naona aibu kwa sababu ninajua bwana Trump ni nani. Yeye ni mbaguzi wa rangi. Yeye ni tapeli. Yeye ni mdanganyifu," alisema wakili huyo wa zamani wa rais wa Marekani.
Katika ushahidi wake huo, Michael Cohen alifichua jinsi Trump alivyomtaka atoe kitita cha fedha kumziba mdomo Stormy Daniels, mwanamke muigizaji wa filamu za ngono, ambaye alikuwa na uhusiano haramu wa kingono na kiongozi huyo ili asiyatangaze hayo hadharani.
Wakili huyo wa zamani wa rais wa Marekani ameongeza kuwa: "Trump alinitaka nimwambie uongo mkewe, na mimi nilifanya hivyo; kumwambia uongo mke wa rais ni moja ya mambo ninayoyajutia sana."
Cohen aidha amekiri kuhusu maelezo ya uongo aliyotoa mbele ya bunge la Marekani la Kongresi na akafichua ukweli ulivyo kuhusu shughuli za kibiashara za Trump nchini Russia.
Amebainisha pia kuwa: "Wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, nilikuwa nikifanya mazungumzo na Warussia kwa niaba ya Trump; lakini yeye alinikazia macho na kuniambia, hana uhusiano wowote wa kibiashara na Russia; na uongo huo huo alikuwa akiwaambia wananchi wa Marekani."
Kufuatia ushahidi huo uliotolewa na Michael Cohen, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi na Mageuzi ya Baraza la Wawakilishi la Marekani, Elijah Cummings amesema, maelezo hayo yamezusha wasiwasi mkubwa kuhusu hadhi ya kisheria ya tabia ya rais wa Marekani.
Cummings amebainisha kuwa, nyaraka na ushahidi uliotolewa na Michael Cohen umezusha wasiwasi wa kisheria na kimaadili kuhusu hatua alizochukua rais wa Marekani kabla na baada ya kuingia Ikulu ya White House.../