Erdogan: Marekani imekasirishwa na Uturuki huru
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema Marekani inaishinikiza nchi yake iache kununua silaha za Russia kwa sababu wakuu wa Washington wamekasirishwa na sera za Ankara za kujitegemea.
Akizungumza mjini Diyarbakir Jumamosi, Erdogan amesema suala pekee si kupinga hatua ya Uturuki kununua mfumo wa ngao ya makombora kutoka Russia unaojulikana kama S-400 bali muhimu zaidi ni kuwa Marekani imekasirishwa na hatua ya Uturuki kuwa na misimamo huru katika masuala ya eneo hasa kuhusu Syria.
Uturuki inasema imewatuma wanajeshi wake Syria kukabiliana na wanagambo wa Kikurdi ambao inasema wanashirikiana na Wakurdi wa Uturuki wanaotaka kujitenga. Hii ni katika hali ambayo Marekani inaunga mkono wanamgambo hao wa Kikurdi jambo ambalo limepelekea kuibuka msuguano baina yake na Uturuki.
Russia imeafiki kuiuzia Uturuki mfumo wa makombora ya kujihami wa S-400 lakini Marekani imepinga vikali suala hilo kwa sababu Uturuki ni mwanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO. Marekani inasema nchi za NATO hazipaswi kununua silaha kutoka Russia jambo ambalo Uturuki imelipinga vikali.
Aidha hatua ya Marekani kukataa kumkamata na kumrejesha nyumbani Fetullah Gullen ni jambo ambalo limeikasrisha Uturuki. Wakuu wa Uturuki wanasema Gullen, ambaye anaishi uhamishoni Pennsylvania, alihusika katika jaribio la kuipindua serikali ya Uturuki mwaka 2016.