Waasi wanaotaka kujitenga Ireland wakiri kutuma mabomu London
Kundi la waasi la Irish Republican Army (IRA), ambalo linataka eneo la Ireland ya Kaskazini lijitenge na Uingereza limekiri kuhusika na utumaji wa vifurushi vya mabomu katika mji mkuu wa Uingereza, London na Scotland.
Polisi nchini Uingereza imesema waasi wa IRA wamethibitisha kwamba walihusika katika utumaji vifurushi vitano vya mabomu mjini London na eneo la Scotland. Polisi wametangaza kuwa, wameweza kupata vifurishi vinne.
Serikali ya Uingereza imekuwa ikidai kuwa waasi wa IRA wameangamizwa, na kwamba wale waliotuma vifurushi hivyo vya mabomu ni kundi jipya la baadhi ya waliokuwa IRA.
Waasi wa IRA walihusika katika vita vya miongo mitatu vya kutaka kujitenga Ireland ya Kaskazini kabla ya kusitisha uasi mwishoni mwa muongo wa 90. Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa kukishuhudiwa harakati mpya za kutaka kujitenga Ireland ya Kaskazini, mkoa ambao wakazi wake hawafurahishwi na utawala wa Uingereza na wanataka uhuru au kujiunga na Jamhuri ya Ireland. Mwaka huu kumuripotiwa mripuko wa bomu na visa viwili vya ufyatulianaji risasi katika mkoa wa Ireland na tukio hili la kutumwa vifurushi vya mabomu limezusha wasiwasi mkubwa Uingereza kuwa yumkini machafuko yakarejea tena katika mitaa ya nchi hiyo.
Makubaliano ya amani yaliyosainiwa Aprili 10 mwaka 1998, kwa kiasi kikubwa yalimaliza rasmi miaka 30 au miongo mitatu ya mgogoro wa Ireland ya Kaskazini ambao ulisabbaisha vifo vya watu wapatao 3,000.

Mgogoro mkubwa ulikuwa ni baina ya Wakatoliki waliopigania Ireland Kaskazini iungane na Jamhuri ya Ireland na Waprotestanti watiifu kwa Uingereza waliotaka Ireland iendelee kuwa sehemu ya nchi hiyo.
Sasa miongo miwili baada ya mapatano ya amani, mojawapo ya mafanikio makubwa ya mpango wa amani kati ya Waprotestanti na Wakatoliki wa kugawana madaraka katika Ireland ya Kaskazini uko mashakani. Utawala katika nchi hiyo ulianguka tangu Januari mwaka 2017 na jitihada za kuurudisha utawala huo zimeshindikana kutokana na tofauti zilizojitokeza.