Kim Jong-un atoa amri ya kuongezwa uwezo zaidi wa hamasa ya jeshi la Korea Kaskazini kumkabili adui
(last modified Sat, 11 May 2019 14:35:56 GMT )
May 11, 2019 14:35 UTC
  • Kim Jong-un atoa amri ya kuongezwa uwezo zaidi wa hamasa ya jeshi la Korea Kaskazini kumkabili adui

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini ametoa amri kwa viongozi wote wa nchi hiyo kuinua uwezo wa hamasa wa jeshi kwa ajili ya kukabiliana na adui.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limetangaza kwamba Kim Jong-un ametoa amri hiyo kufuatia hatua ya Marekani kutwaa meli ya kubeba mizigo ya serikali ya Pyongyang kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo. Kufuatia hatua hiyo kiongozi huyo ametaka kuongezwa zaidi uwezo wa vikosi vya ulinzi katika eneo la Rasi ya Korea na kuwa mstari wa mbele na upande wa magharibi kwa lengo la kutelekeza operesheni za hamasa ya kiulinzi ili kukabiliana na hali yoyote ile ya hatari.

Kim Jong-un akiwa katikati ya askari wa nchi yake

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Korea Kaskazini imetoa ajenda ya vipaumbele muhimu kwa ajili ya kuimarisha zaidi uwezo wake wa kiulinzi. Aidha Kim Jong-un amebainisha kwamba amani na usalama wa kweli vitadhaminiwa kupitia vikosi vya askari wenye uwezo ambao wanaweza kutetea haki ya kujitawala nchi hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, meli iliyokuwa na tani elfu 17 ya Korea Kaskazini iliyosimamishwa mwaka jana nchini Indonesia kwa tuhuma za kubeba makaa ya mawe, ilitwaliwa na Marekani Ijumaa usiku kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imelaani vikali na serikali ya Pyongyang.

Tags