Amri ya Kim Jong-un ya kuimarishwa uwezo wa jeshi la Korea Kaskazini
(last modified Sun, 12 May 2019 10:27:19 GMT )
May 12, 2019 10:27 UTC
  • Amri ya Kim Jong-un ya kuimarishwa uwezo wa jeshi la Korea Kaskazini

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini ametoa amri ya kuimarishwa uwezo wa jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na adui.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limetangaza kwamba Kim Jong-un ametoa amri hiyo kufuatia hatua ya Marekani kutwaa meli ya kubeba mizigo ya serikali ya Pyongyang kwa kisingizio kuwa imekiuka vikwazo vilivyowekwa. Kufuatia hatua hiyo kiongozi huyo amesisitiza udharura wa kuongezwa uwezo wa vikosi vya ulinzi vilivyo katika mstari wa mbele na ngome ya Magharibi kwa lengo la kuwa tayari kutelekeza operesheni za za kiulinzi ili kukabiliana na hali yoyote ile hatari. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Korea Kaskazini imeainisha ajenda yenye kipaumbele muhimu kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi. Kadhalika Kim Jong-un amebainisha kwamba amani na usalama wa kweli utadhaminiwa kupitia vikosi vya askari wenye uwezo ambao wanaweza kutetea haki ya kujitawala nchi hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, meli iliyokuwa na mzigo wa tani elfu 17 ya Korea Kaskazini iliyosimamishwa mwaka jana nchini Indonesia kwa tuhuma za kubeba makaa ya mawe, ilitwaliwa na Marekani Ijumaa usiku kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imelaaniwa vikali na serikali ya Pyongyang.

Maneva ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini, yanatajwa pia na Pyongyang kuwa ni chokochoko dhidi yake

Amri mpya ya Kiongozi wa Korea Kaskazini ya kuimarishwa uwezo wa kiulinzi wa jeshi la nchi hiyo ni sehemu nyingine ya radiamali ya serikali ya Pyongyang juu ya kuendelea mienendo ya uhasama ya Marekani, ukiwemo wa kuvunja mazungumzo ya pande mbili yaliyokusudiwa kutatua mzozo wa nyuklia katika Rasi ya Korea. Katika wiki za hivi karibuni na baada ya kufeli duru ya pili ya mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong-un huko mjini Hanoi, Vietnam, Korea Kaskazini ilianzisha tena majaribio yake ya makombora kwa lengo la kuonyesha kwamba iko makini katika kutetea maslahi yake ya kitaifa katika mazungumzo na Washington, na kwamba haiko tayari kushindwa kidiplomasia na White House. Katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya pande mbili nchini Singapore, Pyongyang iliahidi kusitisha majaribio yake ya makombora na silaha za nyuklia, hata hivyo White House ikakiuka ahadi zake kuhusu kusimamishwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya Asia ambapo ilirefusha kwa kipindi cha mwaka mmoja mwingine vikwazo vyake dhidi ya Korea Kaskazini.

Kim Jong-un akiwa pamoja na askari wa nchi yake

Kuhusiana na suala hilo Pascal Boniface mkuu wa kitivo cha mahusiano ya kimataifa na kistratijia cha nchini Ufaransa anasema: "Marekani ya Trump inadhani kwamba Korea Kaskazini itatokomeza kikamilifu silaha zake za nyuklia, bila ya kuondolewa vikwazo wala kuandaliwa mazingira bora kwa ajili ya uchumi wake. Hii ni katika hali ambayo Pyongyang inasisitiza kuwa bila kuondolewa vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi dhidi yake, kamwe haitatokomeza silaha zake za nyuklia." Ukweni ni kwamba Korea Kaskazini haipo tayari kuendelea kushuhudia ukwamishaji mambo na uvunjaji ahadi wa Marekani kuhusiana na duru mbili za mazungumzo ya hivi karibuni, hasa kwa kuzingatia kuwa katika mazungumzo ya kuangamiza silaha za nyuklia ya huko nyuma yaliyoitwa, mazungumzo ya nyuklia ya pande sita mwaka 2007, Marekani licha ya kutoa ahadi chungu nzima, haikutekeleza hata ahadi moja kati ya ahadi hizo. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndio maana Kim Jong-Un, Kiongozi wa Korea Kaskazini sambamba na kutekeleza siasa za kurejea kwenye ajenda yake ya kuyafanyia majaribio makombora, akawa anaidhihirishia jamii ya kimataifa nafasi haribifu ya White House katika kukwamisha mambo kuhusiana na suala la kutokomezwa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Tags