UN: Kuna uwezekano mkubwa wakati huu wa kutumika silaha za nyuklia
Mkurugenzi wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti wa Upokonyaji Silaha UNIDIR amesema hatari na uwezekano wa kutumika silaha za nyuklia duniani hii leo uko juu kuliko wakati mwingine wowote ule.
Renata Dwan amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na kubainisha kuwa, "Nadhani ni sahihi kufahamika kuwa dunia hii leo iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vita vya nyuklia; na uwezekano wa kutumika silaha za maangamizi za nyuklia uko juu zaidi wakati huu kuliko wakati wowote ule, tokeo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia."
Dwan ambaye anaongoza taasisi hiyo iliyoundwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1980 kwa ajili ya kutathmini hatari inayoikabili dunia kutokana na mashindano ya kijeshi amesema kadhia kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia haijakuwa ikiakisiwa ipasavyo na vyombo vya habari.
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Kamati ya Mahusiano ya Kimataifa ya Bunge la Uingereza ilitoa taarifa iliyoonya juu ya uwezekano wa kutokea vita vya silaha za nyuklia kati ya nchi zenye silaha hizo.
Mkataba unaopinga kutumika kwa silaha za maangamizi uliidhinishwa na nchi 122 katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Julai mwaka 2017, baada ya kufanyika majadiliano ya kina yaliyoongozwa na Austria, Brazil, Mexico, Afrika Kusini na New Zealand.
Hakuna nchi hata moja kati ya tisa zinazomiliki silaha hizo za nyuklia ilishiriki katika mkutano huo, zikiwemo Marekani, Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel.