Apr 19, 2016 07:56 UTC
  • Makumi wauawa katika shambulizi la bomu Kabul, Afghanistan

Makumi ya watu wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika mripuko wa bomu ulioutikisa mji wa Kabul karibu na ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan mapema leo.

Kanali ya televisheni ya Tolo ya nchi hiyo imeripoti kuwa, kwa akali watu 28 wameuawa katika shambulizi hilo la kigaidi na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan amelaani hujuma hiyo ya kigaidi, ambayo kundi la kigaidi na kitakfiri la Taliban limekiri kuhusika nayo.

Habari zinasema kuwa, shambulizi hilo lililenga ofisi za taasisi kuu ya usalama nchini humo. Habari zaidi zinasema kuwa, moshi mzito uliokolea weusi umeonekana ukipaa angani kutoka ubalozi wa Marekani katika mji huo mkuu wa Afghanistan, ambao umepakana na makao makuu ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO nchini humo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesema kuwa, kwa sasa eneo hilo liko chini ya ulinzi mkali na kwamba huenda hujuma hiyo imefanywa na gaidi wa kujitolea muhanga.

Wiki iliyopita, kundi la kigaidi la Taliban lilitangaza kuwa litashadidisha vita dhidi ya maafisa usalama wa nchi hiyo na vikosi vamizi, katika operesheni waliyoipa jina la "Mashambulizi ya Machipuo".

Tags