Wakazi wa mji wa Hiroshima, Japan wafanya maandamano kulaani majaribio ya Marekani ya silaha za nyuklia
(last modified Wed, 29 May 2019 03:50:41 GMT )
May 29, 2019 03:50 UTC
  • Wakazi wa mji wa Hiroshima, Japan wafanya maandamano kulaani majaribio ya Marekani ya silaha za nyuklia

Wakazi wa mji wa Hiroshima nchini Japan wamefanya maandamano kulaani majaribio ya hivi karibuni ya silaha za nyuklia yaliyofanywa na Marekani.

Maandamano hayo yamefanyika katika jengo la kumbukumbu za wahanga wa jinai ya silaha za nyuklia iliyotekelezwa na Marekani mwaka 1945, ambapo wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali zinazolaani vikali majaribio ya silaha za nyuklia ya Washington. Katika maandamano hayo Toshiyuki Mimaki, mwakilishi wa kundi la waathirika wa shambulizi la silaha za nyuklia mjini Hiroshima amewambia waandishi wa habari kwamba licha ya kupitishwa na Umoja wa Mataifa sheria inayozuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia, lakini hadi sasa ulimwengu umefikia nusu pekee ya njia ya kutokomeza silaha hizo za maangamizi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kundi la waathirika wa shambulizi la Marekani la silaha za nyuklia mjini Hiroshima wamepanga kumuandikia barua ya malalamiko na ya kulaani majaribio ya hivi karibuni ya silaha hizo hatari Rais Donald Trump kupitia ubalozi wa Marekani nchini Japan.

Unyama wa kutisha uliofanywa na Marekani mwaka 1945 dhidi ya Wajapan

Inafaa kuashiria kuwa wiki iliyopita, serikali ya Marekani ilitangaza kwamba, mwanzoni mwa mwaka huu iliifanyia majaribio silaha mpya za nyuklia. Kufuatia taarifa hiyo, Kazumi Matsui Meya wa mji wa Hiroshima ametoa radiamali akilaani kitendo hicho na kuongeza kuwa majaribio hayo ya Marekani ya silaha hizo za maangamizi ni kitendo kisichosamaheka. Ameongeza kwamba pamoja na mambo mengine, kitendo hicho kimejeruhi hisia za waathirika wa shambulizi la kinyama la jeshi la Marekani mwaka 1945 nchini Japan. Katika shambulizi la silaha za nyuklia la Marekani kwenye miji miwili ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan kwa akali watu laki mbili na elfu 20 waliuawa kinyama.

Tags