Mahakama: Uingereza imekiuka sheria kwa kuiuzia silaha Saudia
Mahakama ya Rufaa nchini Uingereza imesema kuwa serikali ya London ilikiuka sheria kwa kuiuzia silaha Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen.
Akisoma hukumu hiyo jana Alkhamisi, Jaji Terence Etherton amesema Uingereza imekiuka sheria kwa kuiuzia silaha Saudia, pasina kuzingatia ukiukaji wa sheria za kimataifa na ukanyagaji wa haki za kibinadamu unaofanywa na Riyadh katika vita vyake dhidi ya wananchi wa Yemen. Msemaji wa serikali ya Uingereza amesema hawakubaliana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufaa, na kwamba wataikatia rufaa katika Mahakama ya Juu.
Hivi karibuni, shirika la kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International mbali na kuitaka serikali ya Uingereza isitishe uuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen, lililaani mashambulizi ya muungano huo vamizi dhidi ya hospitali, shule na mabasi yanayobeba wanafunzi wa Yemen. Kwa mujibu wa Vuguvugu la Kupambana na Biashara ya Silaha nchini Uingereza, tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Yemen mnamo Machi mwaka 2015, Uingereza imeiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya mabilioni ya pauni.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), asilimia 43 ya silaha zinazouzwa na Uingereza nje ya nchi zinanunuliwa na Saudia.
Mbali na Uingereza kuuuzia silaha utawala wa Aal-Saud, lakini pia imekuwa ikishiriki moja kwa moja katika vita vya Yemen. Mwezi Machi mwaka huu, gazeti la The Mail la Uingereza lilifichua kuwa, makomandoo watano wa kikosi maalumu cha kijeshi cha Uingereza kinachofahamika kama Special Boat Service (SBS) wamejeruhiwa kwa risasi baada ya makabiliano makali kati yao na wapiganaji wa Ansarullah katika mkoa wa Saada wa kaskazini mwa Yemen.