Wanaharakati wa Ujerumani wamkumbuka "Shahidi wa Hijabu" Marwa el Sherbini
Wanaharakati wa Ujerumani leo Jumapili wanahitimisha warsha zilizoanza Jumatatu iliyopita za kukumbuka mauaji ya mwanamke Mwislamu, Marwa el-Sherbini aliyeuawa kwa kudungwa kisu mara kadhaa ndani ya ukumbi wa mahakama ya mji wa Dresden nchini Ujerumani.
Warsha hizo zimefanyika kwa shabaha ya kuhimiza mapambano dhidi ubaguzi na chuki dhidi ya wageni katika mji huo ambao unahesabiwa kuwa ngome ya harakati ya kibaguzi ya Pegida.
Shughuli za mwaka wa kumi wa kukumbuka mauaji ya "Shahidi wa Hijabu" Bi Marwa el Sharbini, zilijumuisha mikutano ya wanawake ndani ya ukumbi wa mahakama ya Dresden mahala alikouliwa mwanamke huyo wa Kiislamu na kongamano lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji huo.
Mwanamke huyo wa Kiislamu, Marwa el Sharbini aliuawa kwa sababu tu ya kuvaa vazi la hijabu na kwa sababu hiyo amekuwa mashuhuri kwa jina la Shahidi wa vazi la Kiislamu la Hijabu.
Jinai hiyo ya kutisha ilitokea baada ya Mjerumani aliyekuwa na umri wa miaka 28 kwa jina la Alex W. kumshambulia kwa maneno Marwa el Sherbini na kumvunjia heshima kwa matusi kutokana na vazi lake la Kiislamu la hijabu. Tarehe Mosi Julai 2009 Mjerumani huyo alimrukia al Sharbini na kumvua hijabu huku akimwita kuwa ni gaidi. Bibi el Sherbini aliwasilisha mashtaka mahakamani ambako Mjerumani mchokozi alihukumiwa kulipa faini ya Euro 750. Mhalifu huyo alikata rufaa mahakamani na tarehe Mosi Julai 2009 alimshambulia mwanamke huyo aliyekuwa na mimba ya miezi mitatu katika ukumbi wa mahakama ya mji wa Dresden na kumuua shahidi kwa kumdunga kisu mara 18. Mjerumani huyo pia alimjeruhi mume wa mwanamke huyo.
Maafa hayo hayakuishia hapo, bali polisi wa Ujerumani pia alimpiga risasi mbili mguuni mume wa Marwa kwa madai kwamba alidhani ndiye aliyemshambulia raia wa Ujerumani.
Gaidi Alex W. amehukumiwa kifungo cha maisha jela.