Trump na balozi wa Uingereza washambuliana kwa maneno
Rais Donald Trump amemshambulia vikali balozi wa Uingereza mjini Washington aliyemtaja kiongozi huyo wa Marekani kama mtu mtepetevu, asiye na tajriba na anayeendesha Ikulu ya White House kishaghalabaghala.
Trump amesema utawala wake sio katika mashabiki wakubwa wa balozi huyo wa Uingereza mjini Washington, Kim Darroch.
Trump amesema mwanadiplomasia huyo wa UK hajaifanyia haki nchi yake kutokana na matamshi yake dhidi ya uongozi wake.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza limevujisha kanda ya sauti ya balozi huyo wa Uingereza mjini Washington, ambaye amesema kuwa Trump ni mtu asiye na tajriba ya uongozi na huenda akajiangamiza mwenyewe, na yumkini uongozi wake ufikie tamati ghafla.
Mwanadiplomasia huyo wa Uingereza alisema, "Hatuamini kuwa utawala huu wa Trump utabadilika na kuwa wa kawaida. Utawala huo umelemaa, hautabiriki, hauna tajriba, haushauriki na wala hautilii maanani misingi ya diplomasia."
katika kujaribu kupunguza msuguano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Jeremy Hunt amesema "Serikali ya London inaamini kuwa utawala wa Trump unaendesha mambo ipasavyo na ni rafiki wa karibu wa Uingereza katika uga wa kimataifa."