Maandamano ya Vizibao Vyeusi Paris, wakimbizi wa Kiafrika wataka kupewa vibali
Mamia ya wakimbizi wa Kiafrika wanaojulikana kwa jila la Harakati ya Vizibao Vyeusi wamefanya maandamano mjini Paris wakitaka kupewa vibali vya kuishi nchini Ufaransa.
Karibu wakimbizi 300 wa Kiafrika wa harakati hiyo walifanya maandamano jana Ijumaa mjini Paris wakilalamikia hali mbaya inayowasumbua wakimbizi na wahajiri wa Kiafrika nchini Ufaransa.
Wakimbizi hao ambao aghlabu yao ni kutoka nchi za magharibi mwa Afrika, wanataka wapewe vibali rasmi vya kuishi nchini Ufaransa. Vilevile wametaka kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ufaransa, Édouard Philippe kuhusiana na hali na mazingira yao. Wanachama wa harakati ya Vizibao Vyeusi walikusanyika eneo la Panthéon kulikozikwa watu kama Victor Hugo na Émile Zola na kujitangaza kuwa ni watu wanaotambuliwa na Ufaransa kuwa hawana thamani, wasio na vibali vya kuishi nchini humo na ambao sauti zao hazisikiki.
Maandamano hayo ya Vizibao Vyeusi yamepata ilhamu kutoka kwenye maandamano ya Vizibao Vya Njano yaliyoitikisa Ufaransa mapema mwaka huu.
Harakati ya Vizibao vya Njano ilianza kufanya maandamano tarehe 17 mwezi Novemba mwaka jana kupinga mipango ya kiuchumi ya serikali ya Ufaransa ikiwemo hatua ya kupandisha kodi ya nishati na kupunguza ushuru kwa matajiri.