Uchochezi wa mitandao ya kijamii katika nchi zinazopinga sera za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55352-uchochezi_wa_mitandao_ya_kijamii_katika_nchi_zinazopinga_sera_za_marekani
Katika kipindi chote cha utawala wa Rais Vladmir Putin nchini Russia Wamagharibi wamekuwa wakifanya kila wawezalo kuzusha ghasia na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Nchi za Magharibi hususan Marekani, zimekuwa zikitumia zaidi propaganda chafu na vita vya kinafsi dhidi ya Russia na nchi nyingine zisizokubaliana na sera zao za kibeberu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 13, 2019 08:12 UTC
  • Uchochezi wa mitandao ya kijamii katika nchi zinazopinga sera za Marekani

Katika kipindi chote cha utawala wa Rais Vladmir Putin nchini Russia Wamagharibi wamekuwa wakifanya kila wawezalo kuzusha ghasia na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Nchi za Magharibi hususan Marekani, zimekuwa zikitumia zaidi propaganda chafu na vita vya kinafsi dhidi ya Russia na nchi nyingine zisizokubaliana na sera zao za kibeberu.

Maandamano ya hivi karibuni nchini Russia pia yanatajwa kuwa ni sehemu ya mikakati hiyo ya nchi za Magharibi ya kutaka kuzusha ghasia na machafuko katika nchi wapinzani wa sera za kibeberu za Magharibi. 

Katika mkondo huo shirika moja la usimamizi la Russia limeitahadharisha kampuni ya Google baada ya mtandao wa YouTube kuruhusu kuonyeshwa filamu za maandamano haramu yaliyofanyika siku chache zilizopita nchini humo. YouTube ndio mtandao mkubwa zaidi wa pili wa kijamii duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wafuasi na iko chini ya kampuni ya Google. Taasisi ya Roskomnadzor inayosimamia masuala ya mawasiliano, teknolojia ya mawasiliano na vyombo vya habari nchini Russia Jumapili iliyopita iliiitaka kampuni ya Google kusitisha propaganda na matangazo yanayohusiana na maandamano haramu nchini Russia ambayo yanarushwa kupitia mtandao wa YouTube. Shirika la Roskomnadzor limetangaza kuwa: "Iwapo matangazo ya filamu hizo hayatasitishwa katika mtandao wa YouTube, Moscow itaitambua hatua hiyo kuwa ni kuingilia masuala yake ya kiutawala na hatua ya kiuadui." 

Baadhi ya vyombo vya habari hususan vya nchi za Magharibi vimekuwa vikionesha maandamano haramu yaliyofanyika bila ya kibali mjini Moscow baada ya baadhi ya wagombea wa upinzani kukataliwa kugombea katika uchaguzi wa mabaraza ya miji. Awali pia serikali ya Russia iliipiga faini ya karibu dola elfu 11 kampuni ya Google kwa mara ya pili mfululizo kutokana na kukiuka sheria za ndani ya nchi hiyo.

Mitandao ya kijamii inatumiwa vibaya ya nchi za Magharibi kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine

Mitandao ya kijamii kama YouTube imekuwa ikitumiwa vibaya kwa ajili ya malengo mbalimbali ya kifedha, kisiasa, kipropaganda na hata kuhujumu usalama na amani katika nchi na maeneo mbalimbali ya dunia. Suala lililoifanya Moscow iitahadharishe kampuni ya Google ni kuwaruhusu Wamagharibi kutumia vibaya mitandao ya kijamii kama YouTube kwa ajili ya kuathiri mchakato wa kisiasa nchini Russia hususan chaguzi mbalimbali na kuchochea wananchi kufanya machafuko na maandamano kinyume cha sheria.

Utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii hauishii hapo bali pia makundi ya kigaidi yamekuwa yakitumia wenzo huo kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kishetani. Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani wa Uingereza, Ben Wallace anaitaja mitandao ya kijamii kama Facebook na Google kuwa ni "watafuta faida makatili" na kuongeza kuwa: Mitandao hiyo ya kijamii mbali na kusambaza jumbe zisizofaa, haisaidi lolote katika kupambana na mitazamo mikali mitandao na ugaidi."

Wakati huo huo utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii katika nchi zinazopinga ubeberu na udhibiti wa nchi za Magharibi hususan Marekani sasa umechukua sura mpya. Wamagharibi hasahasa Marekani, wamewekeza sana katika mitandao hiyo kwa ajili ya kupeleka mbele malengo yao katika nchi zinazopinga sera zao za kibeberu na wakati huo huo wanawazuia maafisa wa nchi hizo zinazolengwa kuwa na uwezo wa kuingia na kusimamia mitandao hiyo.

Mfano wa wazi zaidi wa mchezo huo mchafu wa nchi za Magharibi ni hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani aliyeyataka mashirika ya teknolojia ya mawasiliano yenye mitandao ya kijamii kuwazuia maafisa wa nchi zinazopinga sera za Washington na nchi nyingine za kibeberu kuwa na kurasa katika mitandao hiyo. Mfano wa karibuni zaidi ni jitihada za Marekani za kutaka Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zariif azuiwe kuingia katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi ameashiria baadhi ya habari zinazohusiana na kufungwa kurasa za Dakta Zarif katika mitandao ya kijamii na kusema: "Suala hilo linaonesha kiwango cha imani ya wasimamizi wa mitandao hiyo kwa uhuru wa kupata habari, uhuru wa kujieleza na kusema."

Kwa kawaida matakwa kama haya ya tawala za kibeberu za magharibi hukubaliwa na wasimamizi wa mitandao hiyo ya kijamii. Kwa utaratibu huo mitandao mingi ya kijamii kama Facebook, Twittew na YouTube ambayo makao na vituo vyao vikuu viko Marekani, sasa imekuwa askari anayehudumia malengo na siasa za serikali ya Washington.