Sanders: Trump ni mbaguzi wa rangi na anapiga vita Uislamu
Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic amesema kuwa Rais wa nchi hiyo, Donald Trump ni mbaguzi wa rangi na anapiga vita dini ya Uislamu.
Seneta Bernie Sanders anayetarajiwa kuchuana na Donald Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani ameiambia televisheni ya CNN kwamba: Uungaji mkono wa Trump kwa marufuku ya Israel inayowazuia wabunge Waislamu Ilhan Omar na Rashida Tlaib wa Kongresi ya Marekani kuingia Israel na Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni kielelezo cha ubaguzi na misimamo yake ya kupiga vita Uiislamu.
Seneta Bernie Sanders ameongeza kuwa, maafisa wa Israel wamechukua uamuzi wa kuwazuia wabunge hao kuingia katika utawala huo na huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kutokana na mashinikizo ya Trump.
Sanders amesema wabunge hao wawili wamezuiwa kuingia Israel licha ya kwamba Marekani inatoa mabilioni ya dola kila mwaka kwa ajili ya kuusaidia utawala huo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala haramu wa Israel Alkhamisi iliyopita ilitangaza kuwa baraza la mawaziri la utawala huo limechukua uamuzi wa kuwazuia wabunge Ilhan Omar na Rashida Tlaib wa Kongresi ya Marekani kuingia Israel kutokana na upinzani wao dhidi ya utawala huo.
Wabunge Ilhan Omar na Rashida Tlaib ndio Waislamu wa kwanza wa kike kuchaguliwa katika Kongresi ya Marekani na walitarajiwa kufanya safari Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na vilevile kuzuru Msikiti wa al Aqsa.
Awali Rais Donald Trump wa Marekani alikuwa ametuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa Twitter akiihimiza Israel kuwazuia wabunge hao Waislamu wa Marekani kuingia katika ardhi zinazokaliwa wka mabavu na utawala huo.
Mbunge Rashida Tlaib ana asili ya Palestina na wazazi wake wangali wanaishi katika Ukingo wa Magharibi.