Marekani yakosolewa kwa kukusudia kuangamiza mfumo wa usalama duniani
Rais Donald Trump wa Marekani amevuruga na kuhatarisha sana usalama wa kimataifa kwa kuendeleza sera zake zenye utata za kukiuka kanuni na mikataba ya kimatafa, hasa ya kujiondoa katika mikataba ya kudhibiti silaha hatari duniani.
Russia na washindani wengine wa Marekani katika uga wa kimataifa wamekosoa vikali sera hizo za Trump na kuzitaja kuwa haribifu.
Kuhusiana na hili, Sergey Naryshkin, Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Kigeni ya Russia-RF (D/SVR)- anaamini kuwa, hatua za kutowajibika za Marekani zinalenga kuangamiza mfumo mzima wa usalama wa dunia na ni jambo ambalo litayachochea madola makubwa katika maeneo mbali mbali kuanza kujizatiti kwa silaha za mashambulizi.
Naryshkin anaongeza kuwa: "Mfumo wa pamoja wa usalama duniani ambao umekuwepo kwa takribani miaka 50 sasa leo unavurugwa na Marekani kwa makusudi na unaelekea kuangamia."
Kwa mtazamo wa afisa huyo wa ngazi za juu wa usalama nchini Russia, sera za Marekani zimejengeka juu ya msingi wa kutaka kueneza satwa yake na kuwa dola lenye nguvu kubwa zaidi duniani na ni kwa mtazamo huo ndio wakuu wa Washington wakathubutu kuchukua hatua za kibabe dhidi ya serikali zingine duniani.
Mtazamo huo wa Marekani hauzingatii uhalisia wa mambo kwani hivi sasa Marekani haihesabiwi tena kuwa dola lenye nguvu zaidi duniani. Na hilo limeshuhudiwa katika miaka ya hivi kairbuni ambapo Marekani imefeli katika jitihada zake za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja za kutekeleza mipango yake dhidi ya nchi kama vile Syria na Venezuela. Ni wazi kuwa zile zama za Marekani kufanya inavyotaka duniani kama dola la kibeberu sasa zimefika ukingoni. Sera za Marekani za kusisitiza kueneza ubabe wake duniani zimepelekea madola mengi makubwa ya kieneo kuanza kuimarisha majeshi yao ili yawe na uwezo wa kujihami na kutekeleza hujuma.
Naryshkin hali kadhalika amebainisha wasiwasi wake kuwa kusitishwa utekelezwaji wa mkataba wa upunguzaji silaha za kistratijia unaojulikana kama Start Mpya (New START) mwaka 2021 ni jambo ambalo litafungua njia kwa Marekani kuanzisha mashindano mapya ya silaha za nyuklia duniani. Anasema hii ni katika hali ambayo Marekani na Russia zina jukumu la kuunga mkono muundo wa mapatano ya kimataifa ya kudhibiti silaha na zinapaswa kuwa vigezo katika maudhi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov mnamo Aprili 13 mwaka 2019 katika kikao cha Baraza la Sera za Kigeni na Ulinzi la Russia alisisitiza kuwa, mashindano ya silaha sasa yanapewa kipaumbele na Marekani lakini Russia haitaingia katika mashindano hayo ya silaha.
Hii si mara ya kwanza kwa sera za utawala wa Trump kukosolewa vikali na maafisa wa ngazi za juu wa Russia.
Muelekeo wa utawala wa Trump wa kuchukua maamuzi ya upande mmoja (unilateralism) pamoja na sera za utumiaji mabavu katika uga wa kimataifa ni nukta ambazo zimevuruga sana mfumo wa kimataifa. Kama ambavyo pia hivi sasa mfumo wa biashara duniani umevurugwa kutokana na vita vya ushuru wa forodha ambavyo Trump amavianzisha na China. Sera hizo mbovu za kibiashara za Trump zimepelekea wakuu wa sekta ya fedha kimataifa hasa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF) kutahadharisha kuhusu kadhia hiyo.
Russia kwa mara kadhaa imetangaza kuwa, utawala wa Rais Trump umekiuka misingi ya sheria za kimataifa na kwamba utawala huo unategemea mbinu kama vile vitisho, vikwazo, na mashinikizo kuyalazimisha mataifa mengine yafuate sera zake.

Sera hizo za Trump zinakosolewa vikali na Russia pamoja na China ambayo ni madola makubwa duniani na ambayo ni washindani wakuu wa Marekani katika uga wa kimataifa. Marekani inapinga vikali kuongezeka uwezo wa washindani wake wakuu hasa Russia na China na pia inapinga mfumo wa kimataifa wa kuchukuliwa maamuzi kwa msingi wa mashauriano ya pande kadhaa (multilateralism). Kwa msingi huo Marekani ingali inajaribu kuwa dola kubwa zaidi la kibeberu duniani ili kwa njia hiyo izilazimu nchi zote zitii matakwa yake.
Pamoja na hayo yote lakini tunashuhudia kuendelea kuporomoka nguvu za Marekani kutokana na sera za Trump za kuchukua maamuzi ya upande moja. Aidha hivi sasa tunashuhudia namna ambavyo hatua kwa hatua dunia imeanza kusimama kidete kukabiliana na sera za Trump za kuvuruga usalama wa kimataifa.