Safari ya Mogherini mjini Havana; sisitizo la ustawishaji uhusiano na Cuba
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55906-safari_ya_mogherini_mjini_havana_sisitizo_la_ustawishaji_uhusiano_na_cuba
Umoja wa Ulaya daima umekuwa ukisisitiza kuhusu kuimarisha uhusiano na Cuba, msimamo ambao unakinzana na sera za Marekani. Katika fremu hiyo Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini Jumapili aliwasili Havana, mji mkuu wa Cuba kwa lengo la kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Bruno Eduardo Rodríguez pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2019 22:05 UTC
  • Safari ya Mogherini mjini Havana; sisitizo la ustawishaji uhusiano na Cuba

Umoja wa Ulaya daima umekuwa ukisisitiza kuhusu kuimarisha uhusiano na Cuba, msimamo ambao unakinzana na sera za Marekani. Katika fremu hiyo Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini Jumapili aliwasili Havana, mji mkuu wa Cuba kwa lengo la kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Bruno Eduardo Rodríguez pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu nchini humo.

Mogherini amewahi kulaani mara kadhaa vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Cuba na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria.

Pamoja na kuanza mchakato wa kuwa  na uhusiano wa kawaida baina ya Marekani na Cuba mwishoni mwa duru ya pili ya serikali ya Obama ikiwa ni pamoja na kufunguliwa tena balozi za nchi mbili, lakini baada ya kuja madarakani Donald Trump Januari 20 mwaka 2017, wakuu wa sasa wa Washington wamechukua misimamo mikali dhidi ya Havana. Sera mpya za Trump zimepelekea kuvurugika tena uhusiano wa nchi mbili. Trump alitupilia mbali sera za Obama za kuboresha uhusiano na Cuba na badala yake kumeshuhudiwa kuvurugika uhusiano huo sambamba na kushadidishwa mashinikizo na vikwazo dhidi ya Cuba.

Pamoja na hayo lakini Umoja wa Ulaya na nchi kubwa za Ulaya kama vile Ujerumani na Ufaransa zimesisitiza kuhusu kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba.

Baada ya mkutano wa Federica Mogherini na Bruno Eduardo Rodríguez mnamo Apirli 24 2019, Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa na kusisitiza kuwa: Moja kati ya ajenda za mkutano huo ni kuhusu uamuzi wa Marekani wa kutekeleza kipengee cha tatu cha Sheria ya Helms-Burton. Umoja wa Ulaya sambamba na kubainisha masikitiko yake kuhusu uamuzi huo wa Marekani unaamini kuwa, kutekelezwa sheria hiyo ni jambo lililo nje ya mamlaka ya Marekani na ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Eduardo Rodríguez

Kipengee cha tatu cha Sheria ya Helms-Burton ambayo ilipitishwa mwaka 1996 inawapa raia wa Marekani uwezo wa kufungua kesi katika mahakama za Marekani kuhusu milki zao zilizotaifishwa na Cuba mwaka 1959. Marais waliotangulia wa Marekani wamekuwa wakijizuia  kutekeleza kipengee cha tatu cha sheria hiyo lakini  mwezi Mei 2019 Trump alichukua uamuzi wa kuanza kutekeleza sheria hiyo.

Uamuzi huo wa Trump umekosolewa vikali na Umoja wa Ulaya. Kama alivyosema Mogherini: "kuweka vivingiti vya upande mmoja dhidi ya Cuba ni kinyume cha sheria za kimataifa na Umoja wa Ulaya utapinga suala hilo."

Umoja wa Ulaya unataka kuwa na uhusiano bora na Cuba na hivi sasa nchi kubwa za umoja huo ni wawekezaji wakuu nchini Cuba hasa katika sekta za utalii na ujenzi wa nyumba.

Disemba mwaka 2016 Mogherini alitembelea Cuba na pande mbili zikatiliana saini mapatano ya 'Mazungumzo ya Kisiasa na Ushirikiano."

Kwa mujibu wa mapatano hayo, msingi mpya wa uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Cuba ulianzishwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara, mazungumzo ya kisiasa na ushirikiano wa kiuchumi.

Mnamo Julai 2017, Bunge la Umoja wa Ulaya liliidhinisha mapatano hayo. Eduardo Perrra, mhadhiri wa chuo kikuu nchini Cuba ameashiria kuhusu mapatano hayo na kusema utekelezwaji wake unaweza kuwa kwa manufaa ya Umoja wa Ulaya na Cuba.

Kupitishwa mapatano hayo katika bunge la Umoja wa Ulaya ni aina fulani ya nchi za umoja huo kubainisha upinzani wao kwa sera za Trump kuhusu Cuba.

Lengo kuu la Marekani katika kushadidisha mashinikizo ya kifedha na kiuchumi dhidi ya Cuba,  ni kuidhoofisha serikali ya mrengo ya kushoto nchini humo na hatimaye kuiangusha.

Rais Trump wa Marekani

Mwezi Mei mwaka 2019, Umoja wa Ulaya ulililalamikia Shirika la Biashara Duniani WTO kufuatia vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Cuba. Umoja huo ulisisitiza kuwa, ili kulinda maslahi ya mashirika yake, utasimama kidete kukabiliana na vikwazo vya Marekani.

Katika kukabiliana na sera haribifu za Trump, Umoja wa Ulaya umeamua kuimarisha maingiliano yake na Cuba na safari za viongozi wa ngazi za juu wa Ulaya  nchini Cuba na kutiwa saini mapatano mbali mbali ya ushirikiano ni ishara ya azma ya Ulaya ya kupinga sera za Marekani katika kadhia ya Cuba.