Bangladesh yataka dunia itatue mgogoro wa wakimbizi Waislamu Warohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56146-bangladesh_yataka_dunia_itatue_mgogoro_wa_wakimbizi_waislamu_warohingya
Serikali ya Bangladesh imetoa wito kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua za kivitendo kutatua mgogoro wa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wamelazimika kutafuta hifadhi nchini humo kutokana na mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekelezwa dhidi yao huko Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 21, 2019 07:10 UTC
  • Bangladesh yataka dunia itatue mgogoro wa wakimbizi Waislamu Warohingya

Serikali ya Bangladesh imetoa wito kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua za kivitendo kutatua mgogoro wa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wamelazimika kutafuta hifadhi nchini humo kutokana na mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekelezwa dhidi yao huko Myanmar.

Bangladesh imesema itawasilisha kadhia ya wakimbizi Waislamu Warohingya katika kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambacho kitaanza Jumanne ijayo mjini New York. Katika kikao hicho, Bangladesh imekusudia kuiomba jamii ya kimataifa ichukue hatua za kivitendo za kuishinikiza serikali ya Myanmar iwaruhusu wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waweze kurejea katika nchi yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh Abul Kalam Abdul Momen katika mahojiano na waandishi habari amesema: "Kushiriki Bangladesh katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa sababu Bangladesh itaweza kuushinikiza zaidi utawala wa Myanmar ili wakimbizi Waislamu Warohingya waweze kurejea katika nchi yao.

Mnamo 25 Novemba 2018, Bangladesh na Myanmar zilitiliana saini mapatano ya kuwawezesha wakimbizi Waislamu Warohingya kurejea katika makao yao mkoani Rakhine lakini utawala wa Myanmar umeweka vizingiti katika utekelezwaji wa mapatano hayo.

Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Bangladesh imeazimia kuiomba jamii ya kimataifa itatue mgogoro wa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar katika hali ambayo hivi sasa kumeshuhudiwa duru mpya ya ukandamizaji dhidi ya Warohingya.  La kusikitisha ni kuwa, jamii ya kimataifa hadi sasa imepuuza maombi ya mara kwa mara ya serikali ya Bangladesh kuhusu kutatuliwa kadhia ya ukimbizi wa Waislamu hao.

Kuanzia Agosti 25 mwaka 2017, Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine nchini Myanmar na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya Mabuddha wenye misimamo mikali na vikosi vya jeshi la Myanmar kuanzisha wimbi kubwa la hujuma, ukandamizaji na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu hao. 

Ata Nurul-Islam Arkani, mtaalamu wa masuala ya Myanmar anasema: "Mgogoro wa sasa wa jamii ya Warohingya ulianza mwaka 2012 na kila siku hali inazidi kuwa mbaya na jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa haujatekeleza majukumu yake kuhusu jamii hiyo. Jamii ya kimataifa imetosheka tu na kutoa taarifa za kulaani lakini haijachukua hatua zozote athirifu na za kivitendo kutatua mgogoro wa Waislamu Warohingya.

Kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinatazamiwa kuhudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa ngazi za juu wa aghalabu ya nchi za dunia na kwa msingi huo serikali ya Bangladesh inatatarajia kuwa, kwa kuwasilisha kadhia ya wakimbizi Warohingya katika kikao hicho na kutoa tahadhari kuhusu taathira mbaya za kupuuza mahitaji ya Waislamu hao wakimbizi, nchi zitakazoshiriki zitaweza kuchukua maamuzi ya kuishinikiza serikali ya Myanmar ili itekeleze mkataba wa kuwaruhusu wakimbizi warejee na wapate mazingira salama.

Kwa mtazamo wa serikali ya Bangladesh, stratijia kuu ya jamii ya kimataifa kuhusu wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya inapaswa kuwa ni kudhamini usalama wao pindi wanaporejea katika ardhi yao ya jadi nchini Myanmar. Kwa msingi huo kunapaswa kuundwe kamati maalumu katika Umoja wa Mataifa ili kuandaa mazingira ya kuishurutisha serikali ya Myanmar iwaruhusu wakimbizi Warohingya waweze kurejea  makwao. Serikali ya Myanmar inapaswa kutoa dhamana kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuandaa mazingira bora ya kuwapokea wakimbizi wanaorejea na kulinda haki zao za binadamu. Kwa hivyo Umoja wa Mataifa unapaswa kuwa na uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya serikali ya Myanmar iwapo itakiuka ahadi zake kuhusu kuwadhaminia usalama na haki Warohingya watakaorejea nyumbani.

Kambi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya katika eneo la Cox’s Bazar nchini Bangladesh

Nukta hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa, wasiwasi mkubwa walionao wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya kuhusu kurejea makwao nchini Myanmar ni kuwa wanajeshi na Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu ada wangali wanaendeleza jinai na hatua zilizo dhidi ya binadamu na hivyo kufanya maisha ya kawaida kwa Waislamu kuwa jambo lisilowezekana.