Kumalizika kusikoeleweka kwa mazungumzo ya biashara kati ya Marekani na China
Siasa za kimaslahi na za upendeleo wa kiuchumi zinazotekelezwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambazo zinalenga kushadidisha mgogoro wa ushuru wa forodha, zimeibua vita vikubwa vya kibiashara kati ya nchi hiyo na China.
Kwa kuzingatia hasara isiyovumilika ya makabiliano hayo ya kibiashara, viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya biashara wa nchi mbili katika ngazi ya manaibu waziri, wamefanya mazungumzo ya siku mbili mjini Washington kwa lengo la kufikia njia ya utatuzi wa mzozo huo, kikao ambacho kilimalizika siku ya Ijumaa bila natija yoyote inayofahamika. Kuna mgongano kuhusiana na matokeo ya mazungumzo hayo. Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, wawakilishi wa China katika mazungumzo hayo ya kibiashara, waliamua kubadilisha ghafla ratiba yao na kurejea nchini kwao kabla ya muda uliopangwa. Kwa mujibu wa Nicole Rolf, mkuu wa masuala ya ndani katika idara ya wakulima ya jimbo la Montana nchini Marekani, wawakilishi wa kibiashara wa China katika mazungumzo hayo walibadili ghafla ratiba yao, sambamba na kuvunja ratiba ya kukutana na wakulima wa Marekani, ambapo walirejea China kabla ya muda uliopangwa. Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu sababu iliyopelekea maafisa hao wafupishe safari yao nchini Marekani. Idara ya kilimo ya jimbo la Nebraska nchini Marekani pia imetangaza kwamba, viongozi wa China walivunja ratiba ya kukutana na wakulima wa jimbo hilo. Kuvunjwa safari hiyo kumevuruga matumaini ya kununuliwa na China mazao ya kilimo kutoka Marekani. Ununuzi wa mazao hayo ulisitishwa kuanzia mwezi Aprili mwaka huu katika kujibu ongezeko la ushuru wa forodha uliowekwa na serikali ya Trump dhidi ya China.
Ukweli ni kwamba wawakilishi wa China katika mazungumzo hayo ya kibiashara na Marekani waliamua kuvunja safari yao na kurejea nchini kwao kufuatia matamshi ya siku ya Ijumaa ya Rais Donald Trump aliyesema kuwa, hatohitajia tena makubaliano yoyote ya kibiashara hadi baada ya uchaguzi wa rais wa 2020. Katika hotuba hiyo Trump alisema: "Ninaamini kuwa kumefanyika kazi kubwa katika sekta za kiuchumi na kijeshi. China imeathirika sana, lakini sisi hatujaathirika." Matukio hayo yamesambaratisha matumaini ya kufikiwa mwafaka wa kibiashara kati ya pande mbili katika siku za usoni, na hivyo kuathiri masoko ya kifedha. Katika upande wa pili, baadhi ya vyombo vya habari nchini Marekani vimeyaeleza mazungumzo hayo kati ya viongozi wa ngazi za juu wa kibiashara wa China na Marekani kuwa yalikuwa chanya na kudai kuwa katika mazungumzo hayo kulijadilikwa kwa njia nzuri masuala ya kiuchumi na kibiashara. Aidha katika kikao hicho pande mbili zilijadili suala la kufanyika duru ya 13 ya mazungumzo ya kibiashara kati ya nchi mbili mwezi Oktoba mwaka huu mjini Washington. Ofisi ya uwakilishi wa kibiashara nchini Marekani imetoa taarifa kuhusiana na mazungumzo hayo ya siku mbili kuwa yalikuwa chanya na kwamba taratibu za kufanyika mazungumzo kwa ngazi ya juu mwezi ujao, zimekamilika. Hata hivyo, licha ya ripoti hizo zinazoonyesha kuwa mazungumzo hayo yalikuwa chanya, lakini kitendo cha ujumbe wa China kuondoka mapema mjini Washington, kinabainisha kutoridhishwa serikali ya Beijing na mwenendo wa kibiashara wa kimaslahi unaotekelezwa na serikali ya Trump.
Kupitia jumbe za mtandao wa Twitter na matamshi yake Trump amekuwa akikariri kuwa China imepata hasara kubwa katika vita vya sasa vya kibiashara na Marekani. Anatekeleza siasa za makusudi za kujaribu kuficha hasara iliyoipata Marekani katika vita hivyo vya kibiashara hususan kwenye sekta ya kilimo ya nchi yake na kuonyesha kwamba Wachina ndio washindwa katika vita hivyo. Wakati huo huo rais huyo wa Marekani anajitahidi kuionyesha China kuwa ni tishio katika uga wa kimataifa ili kwa njia hiyo aweze kuhalalisha hatua zake za kiuhasama dhidi ya nguvu hiyo kubwa ya kiuchumi duniani. Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison siku ya Ijumaa katika ikulu ya Marekani na akijibu swali kwamba ni zipi siasa za baadaye za Marekani katika kukabiliana na mpango wa kuimarishwa uwezo wa kijeshi wa China, Trump alisema: "Bila shaka China ni tishio kwa ulimwengu, kwa kuwa inaimarisha haraka uwezo wake wa kijeshi kuliko nchi zote." Kwa utaratibu huo mbali na kukabiliana na China kibiashara kama moja ya nchi kubwa zenye uchumi wenye nguvu, Trump anajaribu kuidhihirisha nchi hiyo ya Asia kuwa tishio kutokana na uwezo wake mkubwa wa kijeshi ili kwa njia hiyo aweze kuhalalisha hatua za kichochezi na kijeshi za nchi yake dhidi ya serikali ya Beijing hususan katika Bahari ya China Kusini.