Rouhani: Vikwazo vya kikatili vya Marekani vimeongeza mshikamano nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56257-rouhani_vikwazo_vya_kikatili_vya_marekani_vimeongeza_mshikamano_nchini_iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya kikatili vya Marekani dhidi ya Tehran vimeshindwa kufikia malengo yake, na badala yake vimeongeza mshikamano miongoni mwa wananchi wa Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 26, 2019 09:02 UTC
  • Rouhani: Vikwazo vya kikatili vya Marekani vimeongeza mshikamano nchini Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya kikatili vya Marekani dhidi ya Tehran vimeshindwa kufikia malengo yake, na badala yake vimeongeza mshikamano miongoni mwa wananchi wa Iran.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika mazungumzo yake na kikundi cha watalaamu wa sera za nje wa Marekani pambizoni mwa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kufafanua kuwa, "Kinyume na matarajio ya Washington, mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran yameyafanya makundi yote ya kisiasa na kijamii ya Iran kuungana na kuitazama Marekani kama chanzo na matatizo katika nyuga tofauti nchini Iran."  

Amesema makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ndiyo mapatano bora zaidi na ripoti kadhaa za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimethibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu imefungamana na makubaliano hayo, na wala haina azma ya kukiuka hati hiyo ya kimataifa na kanuni zinazohusu miradi ya nyuklia.

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, Iran iko tayari kuidhinisha Protokali ya Ziada kwenye JCPOA kupitia Bunge la Iran na kuwa sheria ya kudumu, mkabala wa Kongresi ya Marekani kuyaidhinisha makubaliano hayo ya kimataifa, sambamba na kuliondolewa daima taifa hili vikwazo. 

Kuhusu migogoro katika eneo la Asia Magharibi, Rais wa Iran amebainisha kuwa, jamii ya kimataifa ina jukumu la kuhakikisha kuwa mashambulizi ya anga yanayofanywa na muungano vamizi wa Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen kwa kutumia mabomu ya Marekani na nchi za Ulaya yanakomeshwa.

Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akihutubia mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kwengineko katika kikao hicho na watalaamu wa sera za nje wa Marekani, Dakta Hassan Rouhani ameeleza bayana kuwa, "Iran haikubaliani na Uzayuni katika hali yoyote ile, ingawaje tuna uhusiano mzuri na Mayahudi. Uyahudi ni miongoni mwa dini takatifu na Qurani Tukufu imewataja Mitume wa Kiyahudi. Tatizo letu ni Uzayuni wenye kiu ya kumwaga damu na kukanyaga haki ya kujitawala jirani zake."

Kadhalika Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa mataifa yote ya eneo hili kuunga mkono mpango wa usalama na amani katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi unaofahamika kama Jitihada za Amani katika Hormuz (Hormuz Peace Endeavor-HOPE).

Ameeleza bayana kuwa, nchi ajinabi hazina nia wala haja ya kuzipatia ufumbuzi changamoto za kiusalama katika eneo hilo kwa kuwa hilo litayatia mashakani maslahi yao ya kuuza silaha.